Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Shamimu Mwariko amesema kutokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) ni dhahiri kwamba lengo la 80% ya wananchi kutumia nishati hiyo litafikiwa ifikapo Mwaka 2034.
Amesema hayo Agosti 15, 2025 wakati wa kutambulisha mradi wa kusambaza majiko ya gesi ya kilo 6 na vichomeo vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 kwa jiko unaoratibiwa na REA na kutekelezwa na Mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited iliyoshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo katika Mkoa wa Katavi.
Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kuhakikisha kwamba Tanzania inaningia, inasimamia na inaishi katika mazingira ya Nishati Safi.
Alibainisha kuwa Halmashauri ya Mpimbwe tayari imeanza uhamasishaji wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa taasisi zinazotoa huduma ya chakula kwa watu wake zikiwemo shule za msingi na sekondari na kwamba baadhi ya shule ikiwemo shule ya Sekondari Mizengo Pinda tayari imefungiwa mfumo wa Nishati Safi ya Kupikia.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majimoto, Seltus Mwanampemba alisema tunayo haja ya kutoka kwenye nishati chafu kwenda kwenye nishati safi kwani matumizi ya gesi yanasaidia kuokoa gharama mfano unapotumia mkaa kama ulitaka kuchemsha kikombe cha maji ule mkaa ndio umeupoteza maana yake unatumia gharama kubwa kwa kazi ndogo.
Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Majimoto, Dakson Schula alimshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha shule hiyo kupata nishati safi ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi.


0 comments:
Post a Comment