Wednesday, January 3, 2018 Waliochoma kanisa la EAGT Bukoba wafungwa kifungo cha maisha jela


Mahakama  ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Bukoba, imewahukumu kifungo cha maisha watu watatu, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa mawili, likiwamo la kuchoma moto kanisa.

Kanisa lililochomwa moto na watu hao ni la Evangelical Assemblies of God (EAGT) mjini Bukoba mkoani Kagera.

Waliotiwa hatiani na Hakimu wa Mahakama hiyo, Charles Oisso ni Rashid Athuman, Ngesella Ismail na Allyu Dauda Hessein.

Hakimu Oisso alisema kuwa watu hao wametiwa hatiani kwa makosa mawili, la kwanza ni kula njama za kutenda kosa walilohukumiwa kifungo cha miaka saba, na la pili ni kutenda kosa la kuchoma kanisa la Evangelical Assemblies of God (EAGT) lililoko mtaa wa Omukibeta Kata ya Kibeta katika Manispaa ya Bukoba.

Alisema kuwa aliwatia hatiani kutokana na washtakiwa hao kuonyesha vitendo vya chuki dhidi ya dini nyingine.

Hakimu Oisso alisema kuwa maeneo ya ibada inabidi yawe salama, maana siyo sehemu ya kujengea watu hofu.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Serikali, Haruna Shomari, awali aliiomba mahakama hiyo kuwapa adhabu kali washtakiwa hao, ili kukomesha vitendo vya aina hiyo, ambavyo alisema vinajenga hofu kwa jamii.

Mwaka 2015, washtakiwa hao walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuchoma moto kanisa hilo ambalo liliteketea pamoja na vitu vilivyokuwamo, na kufikishwa mahakamani mwaka huo.
Share on Google Plus

About KAPOLA NEWZ TV..✍️

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment