Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF) Selemani Bungara maarufu kama Bwege amesema endapo Serikali haitatoa asilimia 65 ya mauzo ya korosho nje ya nchi kwa wakulima wa mikoa ya Kusini hadi Juni 30 mwaka huu wakulima na wabunge wataandamana.
Akichangia bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 bungeni leo juni 20 2018, Bungara amemuomba Spika wa Bunge Job Ndugai kuyapokea maandamano hayo.
Amesema yeye akiwa mwenyekiti wa wabunge wa mkoa wa Lindi wamekuwa wakikaa pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzungumzia mambo yanayowahusu na ndio maana hivi sasa mambo ndani ya mkoa huo yanakwenda vizuri.
“Hii ni kwa sababu tuko wabunge wanne wa upinzani na nyie mko wanne, ngoma droo. Lakini kuna njama ya makusudi inayofanywa na Serikali ya CCM ya kuturudisha nyuma kwa makusudi na sisi hatukubali,”amesema.
Amesema kuwa wanapata ushuru wa huduma kutoka katika miradi ya gesi lakini Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango anataka kupeleka mabadiliko ya sheria ili kuwanyang’anya ili mikoa hiyo ya Kusini irudi nyuma kiuchumi.
Amesema kuna suala la fedha za korosho ambazo Serikali inatakiwa kurudisha asilimia 65 ya mauzo ya korosho nje ya nchi na kwamba mwaka wa fedha 2017/18 walikuwa wanatakiwa kuwarudishia wakulima hao Sh 81 bilioni lakini hadi leo haijafanya hivyo.
“Mheshimiwa Spika ikifika Juni 30 kama hela haijatoka uje (Ndugai) upokee maandamano yetu maana Serikali ya CCM inafanya kazi kama patasi ambayo haifanyi kazi mpaka igongwe. Wabunge wa mkoa wa Lindi tutaandamana hadi asubuhi ili mtoe fedha zetu,”amesema.
Amesema endapo Serikali haitatoa fedha hizo hadi kufikia muda huo varangati kama lililokuwa wakati wa miradi ya gesi inaanzishwa litaanza upya katika mikoa hiyo.
“Wabunge wa mikoa ya Kusini tuungane tupambane huyu Mpango (Dk Mpango) ana matatizo sana,”amesema.
Ameshauri bajeti iongozewe katika mifugo, kilimo na maji na kwamba kama wakiongeza bajeti katika maeneo hayo kwa mara ya kwanza ataiunga mkono bajeti hiyo.
Amesema anajua kuwa wataongeza mishahara na fedha za kilimo mwaka 2019 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ili wachaguliwe katika nafasi zao.
“Mwaka 2019 ndio mtaongeza bajeti kwa wakulima na mishahara kwa wafanyakazi ili wawapigie. Nyie wajanja mnatuua mwishoni. Miaka mitano mnawaacha wapate tabu,”amesema.
0 comments:
Post a Comment