Nyumba Ya Tungo Na Simulizi.sehemu ya kwanza.

RIWAYA: WHERE IS MY JONI?
MTUNZI: KELVIN KAGAMBO
SEHEMU YA KWANZA (1)
Yuko wapi Joni wangu?
Namtafuta nimuombe msamaha. Nimueleze ukweli kuwa shida na mahangaiko nipatayo ni kwasababu yake. Bila shaka Mungu Mwenyezi amezipokea dua zake.
Namtafuta nimwambie kuwa yeye ni mwanaume pekee aliyenifanya niwe mwanamke kamili. Aliyehakikisha jasho lake linatimiza ndoto zangu. Nimueleze kuwa yeye ni Mfalme aliyenifanya Malkia. Kapuku aliyenitajirisha kwa huba la dhati toka uvunguni mwa moyo wake. Akanithibitishia kwa vitendo kuwa ana vigezo vyote vya kuitwa shujaa. Shujaa wa maisha yangu, aliyekubali kuwa mtumwa wangu, akathubutu hata kuweka roho yake rehani kwasababu yangu.
Nakumbuka aliingia Dar es Salaam akitokea Tanga, alikuja hapa kwa kaka yake Gilbert ambaye alikuwa ni mpangaji mwenzetu kwenye nyumba kuu kuu ya Mzee Kiloko; Mzee ambaye anajulikana Temeke nzima kwa ulevi wa mataputapu na chang'aa.
Akishalewa ni vurugu, fujo na matusi ya nguoni huyamwaga hadharani bila kujali chochote.
Kaka yake alikwenda kumpokea ubungo na hata sisi alituaga.
"Nakwenda Ubungo kumpokea mdogo wangu, anaitwa Joni na anaingia leo kutoka Tanga" alituambia.
Baadaye alirejea akiwa na huyo Joni, mvulana mweupe, mrefu na mwembamba. Sitaki kumuongelea sana muonekano wake ila kwa kifupi ni kwamba hakuwa na tofauti sana na vijana wa hapa mjini na pengine ni kwasababu hakuwa akitokea Tanga vijijini.
Kaka yake alimtambulisha kwetu na tangu hapo Joni akawa ni mmoja wa watu waishio kwenye Jumba chakavu la mstaafu Mzee Kiloko.
Wiki tatu zilikatika lakini bado Joni hakuwa mwenyeji, sikuwahi kupata bahati ya kuzungumza naye hata kwa sekunde kumi ingawa mlango wa chumba chao na chetu ilikuwa mkabala (Inatazamana).
Siku hiyo nikiwa ndani, chumbani kwetu nilisikia mtu akibisha hodi. Nikanyanyuka na kwenda kumtazama. Sikuamini nilipofungua mlango na kukuta kuwa aliyekuwa akibisha hodi ni Joni.
"Joni!? Mambo?" nikamsalimu.
"Poa, eti Kaka ameacha funguo yetu huku?" akaniuliza.
"Ndiyo ameacha ngoja nikuchukulie ndani" nikamjibu kisha nikamuacha amesimama pale, nikaingia ndani kumchukilia funguo na punde nikatoka nikiwa nayo; Nikamkabidhi.
"Asante, halafu simu yako ina vocha?" akaniuliza.
"Mimi sina simu, vipi kwani?"
"Aaah basi, nilikuwa nataka niji-beep kwasababu nimepoteza simu yangu"
"Heee! Pole jamani, umepotezea wapi?"
"Sifahamu lakini mara ya mwisho kuwa nayo ilikuwa ni muda mfupi kabla sijapanda gari. Nilipopanda tu sikuiona tena" alivyonambia hivyo tu nikajua kuwa nilazimwa atakuwa ameibiwa kwa mtindo wa ndolema a.k.a Chadema.
Ni mtindo wa wizi ambao umeenea sana huku Dar es Salaam.
Wezi hujifanya ni abiria wanaogombania kuingia kwenye daladala na wanatumia mwanya huo kuchomoa pochi na simu za abiria.
"Ngoja nikuazimie ya Mama basi ujaribu" nikamwambia na kuingia ndani kufuata simu ya Mama.
Punde nilitoka nikiwa nayo na kumpa, akajipigia lakini haikuwa ikipatikana na pengine ilishazimwa na mtu aliyekuwa nayo.
Urafiki wangu na Joni ukaanzia hapo, tukawa tunapiga stori ndogo ndogo kila tunapopata muda.
Safari moja huanzisha nyingine, stori ndogo ndogo nilizokuwa nikipiga na Joni zilizaa stori kubwa na hatimaye tukawa watu wa karibu kabisa.
Majirani wengine wakaanza kuponda na kusema kwamba mimi na Joni tulikuwa na ajenda za mapenzi, haikuwa kweli lakini hiyo ilikuwa ni kawaida ya waswahili, hawaamini kwamba mwanamke na mwanaume wanaweza kuwa na ukaribu usiohusisha mapenzi.
Lakini nahisi lisemwalo lipo na kama lipo laja, mimi binafsi nilianza kutamani kuwa na mahusiano na Joni. Nilitamani awe mpenzi wangu tena kweli kweli, nimpe moyo wangu akae nao na kuutunza.
Lakini naanzia wapi ikiwa mimi ni mwanamke tu, na kama unavyojua kuwa mwanamke kumtongoza mwanaume ni sawa na kufanya shambulio la kujitoa mhanga, yaani kunahitaji ujasiri na kujitoa.
Joni mwenyewe hakuwa hata na ishara zozote za kutaka kuwa na mahusiano na mimi, alionekana kuupenda ule urafiki zaidi.
Lakini nilishindwa kuvumilia, Joni alinikaa moyoni na ikanibidi nimwambia ingawa si kwa kutumia mdomo.
Nilimuandikia kibarua ambacho kilibeba maelezo yote kuhusu hisia zangu juu yake. Humo nilimueleza kwamba nampenda na nimeamua kumwambia baada ya kuona nateseka kwa muda mrefu sasa.
Sifahamu alikuwa katika hali gani pindi alipokuwa akisoma barua hiyo lakini naamini kama alikuwa akinipenda basi alifurahi sana.
Naye pia aliniandikia barua, barua ambayo ilibeba majibu ya kile nilichomueleza. Nashukuru kwamba barua hiyo ilikuwa na sentensi inayosomeka "Hata mimi nakupenda sana Hellen" lakini nilikosa nguvu na matumaini baada ya sentensi hiyo kufuatiwa na neno "Lakini" halafu ikaendelea kwa kusema "Hellen mimi sina pesa ya kuendesha mahusiano, ndiyo kwanza nimekuja kwa kaka anitafutie kibarua au hata shule ya ufundi nikasome ili nipate ajira ya kuanza maisha hapa Dar es Salaam, unadhani ni vipi nitakuhudimia?" akanambia, lakini hakufahamu tu kwamba mimi nilikuwa nampenda kwa mapenzi, yaani hata asingekuwa na hiyo pesa anayoisema nampenda tu.
Isitoshe mimi bado ni mwanafunzi, nimemaliza kidato cha nne na sasa niko nyumbani nasubiri matokeo kwahiyo sidhani kama nina mahitaji makubwa ya kiasi cha kumuumiza kichwa.
Naishi na mama yangu tu hapa tulipopanga, mama si tajiri lakini anajitahidi kunihudumia kwa vitu muhimu kwahiyo sidhani kama tutashindwa kuwa wapenzi kwasababu hiyo.
Nilimuandikia Joni kibarua kingine chenye kumueleza hayo na hiko kilikata mzizi wa fitina kwani Joni kwani alinikubali moja kwa moja na tukawa wapenzi.
Ingawa watu wanasema eti kuishi na mpenzi wako karibu namna hiyo haipendezi kwasababu mnakosa hata ku-miss-ana lakini mimi napinga. Napinga kwasababu ingawa muda mwingi nilikuwa nikikaa naye lakini nilim-miss hata kwa sekunde kadhaa alizokuwa mbali nami.
Nilimpenda Joni na nasadiki upendo wa namna ile ungedumu basi angelikuwa ni mwanaume aliyepata bahati ya kupendwa kwa dhati zaidi ya wote hapa duniani.
************************************
"Wakati nahangaika kuchangachanga hela zangu nifyatue matofali wewe ulikuwa unafanya umalaya tu, halafu leo unanibania pua eti oooh, sina hela naomba univumilie wiki moja. Ina maana wewe huna bwana wa kukupa hela ya kodi, wanaku**mba kwa mkopo au?" alipiga kelele za namna hiyo mzee Kiloko.
Hapo alikuwa ameshalewa chakali pombe za mataputapu na chang’aa na maneno hayo alikuwa akimwambia Mama yangu.
Nilijisikia vibaya sana kwani yalikuwa ni matusi ya nguoni na aliyetoa bila kujali kundi la watu waliojazana kufuatili mtiti huo.
Mama yangu aliahibika sana, alikuwa amesimama kwa huruma na unyonge huku Mzee Kiloko akimporomoshea mvua hiyo ya matusi yenye kawaida ya kunyesha bila mawingu.
Mimi nilikuwa ndani nikilia, sikutegemea kama mama yangu angekuja kudhalilika kwa kukosa elfu arobaini na tano tu ambayo ni kodi ya miezi mitatu.
Hakuwa nayo, kwani siku mbili zilizopita wagambo wa jiji walimvamia eneo ambalo anafanyia biashara na kumsweka ndani. Ikabidi atoe hongo ili aachiwe huru lakini pesa pekee tuliyokuwa nayo ndiyo hiyo shilingi elfu arobaini na tano ambayo ilikuwa mahususi kwa kumlipa mlevi mbwa; Mzee Kiloko.
Kwahiyo akawa amepotoze mtaji wote wa mama n'tilie aliokuwa nao na kitu pekee alichokuwa akitegemea ni pesa ya upatu ambayo angeipokea wiki moja baadae na hapo ndipo angeanza tena biashara na kupata hela ya kumlipa Mzee Kiloko.
Nikiwa ndani nasikiliza jinsi chapombe Kiloko anavyomdhalisha Mama yangu mlango ukagongwa. Nikawa najishauri kuinuka na kwenda kuufungua kwani nilihisi aibu ya kuonana na mtu yeyote yule.
Ila hodi ilipozidi nilijikuta nimenyanyuka na kwenda kufungua na hapo nikakutana na Joni.
"Hellen, kuna nini?" akaniuliza kwani hakuwepo nyumbani. Kwa kweli nikashindwa kumjibu badala yake nikawa nalia tu kwa uchungu.
"Hellen, naomba unyamaze mpenzi wangu, nieleze tatizo ni nini?" akanambia nami nikajikuta namjibu.
"Mama...anatu...kanwa...kwasab...abu haja...li..pa kodi" nikamwambia huku kwikwi za kilio changu zikiharibu mtiririko wa sentensi yangu.
"Shilingi ngapi anadaiwa?" akaniuliza Joni ingawa nilijua haitasaidia kitu hata kama nitamjibu kwani hakuwa na kazi kwahiyo sidhani kama anaweza kuwa na pesa.
"Elfu arobaini na tano" nikamwambia.
"Haya nyamaza basi, ngoja nakuja" akanambia huku akiniacha na kuondoka zake kuingia chumbani kwao.
Punde akatoka akiwa na pesa mkononi, akaja hadi pale nilipokuwa nimesimama na kunipa.
"Chukua nenda kamlipe" akanambia.
Sikuamini kama Joni angekuwa na pesa, pesa ambayo pengine ingemsaidia Mama yangu kuondokana na mzigo wa aibu uliokuwa juu yake.
Sikutaka kujishauri wala kujiuliza, nilichofanya ni kuipokea ile pesa toka kwa Joni na kutoka hadi barazani ambapo nilimsogelea Mzee Kiloko na kumpa.
"Chukua hela yako na uende, tumechoka kelele zako" nikamwambia. Pengine hata Mama alishangaa sana na kujiuliza ni wapi nimepata pesa hiyo.
Akaichukua na kuhesabu kisha kuitosa kwenye mfuko wa shati lake lilimvaa kwa kukonda kutokana na kunywa chang'aa bila kula chakula kwa ratiba ya kibanadamu.
"ku**nyoko, hamlipi kodi hadi mtiwe vidole....na hii ndiyo dawa yenu, mkichelewa kulipa kodi hata kwa sekunde moja tu nawafuata" akasema na kuondoka.
***********************************************
KAZI MPYA, SEHEMU YA PILI IPO KWA AJILI YAKO, USIKOSE.
Share on Google Plus

About KAPOLA NEWZ TV..✍️

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment