UTEUZI WA RAIS MAGUFULI KUPINGWA MAHAKAMANI Kapola Monday, October 09, 2017


Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kusikitishwa na uteuzi wa Rais John Magufuli wa Katibu wa Bunge.


ACT katika taarifa yake jana Jumapili, imesema Rais ameamua kuyaweka pembeni matakwa ya sheria yanayoongoza mchakato wa uteuzi wa Katibu wa Bunge na kuamua kujichagulia apendavyo.


“Kutokana na unyeti wa nafasi ya Katibu wa Bunge, na kwa minajili ya kuweka 'check and balance' pamoja na kulinda uhuru wa Bunge, kwenye mchakato wa uteuzi wa nafasi husika, sheria imeweka utaratibu wa kufuatwa kwenye uteuzi wa Katibu wa Bunge,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Ado Shaibu ambaye ni katibu wa itikadi, mawasiliano na uenezi wa ACT Wazalendo.


Amesema mbali na Rais kuwa na mamlaka ya kumteua Katibu wa Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 87 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, anapaswa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Sheria ya Utawala wa Bunge ya mwaka 2015.


Kwa mujibu wa kifungu cha 7(3) cha sheria hiyo, Rais atateua jina moja kutoka miongoni mwa majina matatu yaliyopendekezwa na Tume ya Huduma za Bunge.


Shaibu amesema jambo hilo si la hiari bali ni sharti la lazima la sheria ambalo Rais analazimika kulifuata.


Ndiyo maana kifungu husika kinasema, “The Commision shall recommend three names. (Tume ni lazima ipendekeze majina matatu)”.


ACT imesema wajumbe wa Tume ya Huduma za Bunge kwa taarifa ambazo chama hicho kinazo, hakuna kikao chochote kilichoketi na kupendekeza majina kwa Rais kwa ajili ya uteuzi wa Katibu wa Bunge.


Chama hicho kimesema uteuzi huo ni ushahidi wa wazi wa kudharauliwa mhimili wa Bunge.


“Ni matumaini yetu kuwa Bunge na watu wote wanaopenda uhuru na uimara wa Bunge watasimama imara kuupinga uteuzi huu ambao ni kinyume cha sheria,” amesema.


ACT imesema iwapo Rais hatatengua uteuzi huo na kufuata utaratibu uliowekwa na sheria za nchi, kitalifikisha suala hilo mahakamani ili kupata ufafanuzi wa Mahakama.


“Ni wakati muafaka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mwenye dhamana ya kuishauri Serikali kwenye masuala ya kisheria kuwajibika,” imesema taarifa hiyo.
Share on Google Plus

About KAPOLA NEWZ TV..✍️

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment