Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Aidha Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha mkoa wetu unakua mahala salama. Hata hivyo kumekuwa na matukio kama ifuatavyo:-
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WATATU WAKIWA NA NYARA ZA SERIKALI.
Mnamo tarehe 05 Februari, 2018 majira ya saa 19:45 usiku huko maeneo ya Mwanjelwa, Kata ya Ruanda, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya likiwa katika majukumu yake ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na nyara za Serikali ambazo ni vipande vinne vya meno ya Tembo.
Watuhumiwa waliokamatwa wamefahamika kwa majina ya 1. KENEDY LUPEMBE SIMSOKWE [43] Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT – Tawi la Mbeya na Mkazi wa Iyela 2. MATHEW ELIKANA MWANJALA [42] Mpiga picha na Mkazi wa Iyela na 3. SHABAN MKWICHE [24] Mkazi wa Iyunga.
Aidha baada ya kukamatwa na kupekuliwa, watuhumiwa walikutwa na nyara hizo [Vipande vinne vya Meno ya Tembo] ambavyo vina uzito wa kilogram 5 na thamani ya Tshs 33,000,000/=.
Taratibu za kisheria zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani kwa hatua zaidi.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwa na tamaa ya kujipatia utajiri wa haraka kwa kutumia njia za mkato zisizo halali, badala yake wafanye kazi halali ili kupata kipato halali. Aidha Kamanda MPINGA anatoa rai kwa yeyote mwenye taarifa juu ya mtu/ watu au kikundi /mtandao wa watu wengine wanaojihusisha na matukio ya ujangili wazitoe katika mamlaka husika ili hatua za kisheria dhidi yao zichukuliwe mara moja.
Imesainiwa na:
[MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
0 comments:
Post a Comment