Friday, November 2, 2018 Mwanafunzi Atishia Kujinyonga Kisa Kulazimishwa Kwenda Shule


Mwanafunzi wa kike (15) aliyekuwa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Nsemlwa, Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi amenusurika kujiua kwa kujinyonga baada ya baba yake Bushiri Joseph, kumuwahi akiwa tayari amepanda juu ya kiti baada ya kulazimishwa kuendelea na masomo.

Mwanafunzi huyo pamoja mwenzake wa kiume mwenye umri wa miaka 16, anayesoma kidato cha pili katika shule hiyo, wanadaiwa kuwa watoro sugu na kutishia kujiua kwa kujinyonga kwa kamba au kunywa sumu iwapo wazazi na walimu wao wataendelea kuwalazimisha kuendelea na masomo.

Licha ya kuhojiwa na wazazi na walimu wao, wanafunzi hao hawakuwa tayari kueleza kinachowasababisha wakatae kuendelea na masomo na badala yake wamekuwa wakitishia kujiua kama watalazimishwa kurejea shuleni.

Inadaiwa kuwa wazazi wa wanafunzi hao wameshawafikisha kituo cha polisi bila mafanikio, wakiwa na msimamo wao wa kujiua.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Edgar Mwaisunga, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwanafunzi huyo alifikishwa na baba yake mzazi shuleni hapo kujiunga na kidato cha kwanza Januari, mwaka huu.

"Baba yake alikuwa amemnunulia kila kitu alichohitaji binti yake, lakini miezi miwili baadaye alianza utoro, tukimhoji alikuwa akidai kuwa hataki kuendelea na masomo...tulidhani kuwa ni mjamzito, lakini alipopimwa hakuwa na ujauzito,” alisema.

Alisema walimu walijitahidi kumsihi, lakini msichana huyo alikataa kata kata kuendelea na masomo...lakini alikuwa haelezi kwanini hataki kuendelea na masomo, huku akitishia kujiua kama atalazimishwa kuendelea na masomo," alisema.

Kwa mujibu wa Katibu wa Baraza la Kata ya Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Mpanda, Salum Msimani, wanafunzi hao wawili ni miongoni mwa 17 wa Shule ya Sekondari Kasimba, Manispaa ya Mpanda, waliofikishwa katika Baraza la Kata na kufunguliwa mashtaka ya utoro shuleni.

"Wanafunzi hao msichana na mvulana waliokuwa wakisoma katika Shule ya Sekondari Nsemlwa, wakiwa na wazazi na walezi wao walifikishwa wiki iliyopita kwenye Baraza la Kata la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Mpanda na kusomewa mashtaka yao baada ya mkuu wao wa shule na bodi ya shule hiyo kuwasilisha malalamiko dhidi yao na wazazi wao kwenye baraza hilo," alieleza Msimani.

Msimami alisema wanafunzi hao wakiwa kwenye baraza hilo waliendelea na msimamo wao wa kukataa kuendelea na masomo, huku wakisisitiza kuwa kama watalazimishwa kuendelea na masomo watajiua kwa kujinyonga kwa kamba au kunywa sumu .

Alisema, walipotakiwa kueleza sababu zinazowafanya wakatae kuendelea na masomo hawakuwa tayari kuzieleza.

"Baraza hili limeshindwa kutoa hukumu dhidi ya wanafunzi hawa wawili na hata shuleni walikokuwa wanasoma walimu wameinua mikono, pia polisi wamefikishwa na wazazi wao, lakini imeshindikana wameng'ang'ania msimamo wao,” alisema na kuongeza:

“Kama Katibu wa Baraza hili la Kata natarajia kuonana na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda kwa ushauri wa kisheria," alisisitiza.

Aidha, alieleza kuwa kamba aliyotaka kujinyongea mwanafunzi wa kike na kiti alichokuwa amepanda, vipo katika ofisi za baraza hilo.

Baba mzazi wa mwanafunzi huyo wa kike, Bashir Joseph, amedai kuwa hivi karibuni alipomlazimisha binti yake kwenda shuleni aligoma na kuingia chumbani kwake alikokuwa ametundika kamba ya kujinyongea na kumkuta akiwa amepanda kwenye kiti tayari kwa kujinyonga.

Naye baba mzazi wa mwanafunzi wa kiume, Sadok Isha, amedai kuwa pamoja kuchukua hatua mbalimbali za kumfanya kijana wake huyo aendelee na masomo, lakini imeshindikana baada ya kutishia kujinyonga.

Diwani wa Kata ya Uwanja wa Ndege, Stephano Asalile, alisema kwa tukio la wanafunzi hao wawili linaonyesha jinsi ambavyo baadhi ya wazazi wa wanafunzi wamekuwa wakipewa adhabu kutokana na utoro wa watoto wao, kumbe tatizo lipo kwa watoto wenyewe.

Share on Google Plus

About KAPOLA NEWZ TV..✍️

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment