Wananchi Rukwa kushiriki kuchangia Damu kusaidia Majeruhi ajali ya Morogoro


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa mkoa huo kushiriki katika zoezi la kuchangia damu litakalofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 14 hadi 18.8.2019 katika halmashauri nne za mkoa, ili kusaidia majeruhi walioungua na moto uliosababishwa na kulipuka kwa lori la Mafuta katika ajali iliyotokea eneo la Msavu mkoani Morogoro, na kusababisha vifo vya watu 76 na majeruhi 54.
Mh. Wangabo amesema kuwa zoezi hilo litawajumuisha Waendesha Bodaboda na Bajaji, Madereva wa Magari, Vijana, Watumishi wa Serikali, Wanafunzi, Vyama za Siasa, Madhehebu ya Dini, Viongozi mbalimbali na wale wote wenye mapenzi mema na moyo wa kujitolea kwaajili ya majeruhi hao.
“Nafahamu kuwa mtu yeyote aliyeungua sehemu yoyote ya mwili, miongoni mwa madhara makubwa anayoyapata ni pamoja na kupoteza kiasi kikubwa cha maji mwilini (Dehydration) na kupungukiwa damu mwilini (Anaemia).  Kwa hiyo natoa wito na kuwaomba Wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuchangia Damu kwa ajili ya wenzetu majeruhi wanaoendelea na matibabu.  Damu hiyo pamoja na salamu zetu za pole tutaiwasilisha kwa Dkt. Kebwe Steven Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,” Alisema.
Aidha Mh. Wangabo kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Rukwa anaungana na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Viongozi wa Mkoa huo, Familia za Marehemu, Ndugu, Jamaa na Marafiki kwa kuondokewa na Wapendwa wao.  Na kumuomba Mwenyezi Mungu awape Moyo wa Subira na Uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Mungu awape pumziko la milele waliopoteza uhai na awaponye Majeruhi wote wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.  ‘Bwana Alitoa na Bwana Alitwaa Jina lake lihimidiwe’.” Alimalizia.

Mh. Wangabo ametoa maelekezo hayo kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza la madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini.
Share on Google Plus

About KAPOLA NEWZ TV..✍️

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment