Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amevitaka vyama vya ushirika katika Mkoa wa Rukwa kujiunga na chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa ili kuwa na umoja na nguvu katika kutafuta masoko ya mazao yao, kuachana na walanguzi, kulima kwa tija na kuzalisha mazao bora kwa kupata pembejeo kwa wakati na hatimae kufanya kazi kwa karibu na wataalamu wa kilimo waliomo ndani ya mkoa.
Amesema kuwa chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa Ufipa Cooperative Union Ltd (UCU) ni chama kipya na kinahitahi nguvu ya vyama vya ushirika vya mkoa mzima ili kiwe na uongozi uliokamilika, kiweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuweza kumnyanyua mkulima wa mkoa wa Rukwa kutoka alipo sasa na kuwa wakulima wa hadhi ya kimataifa.
“Mkulima ana mahangaiko makubwa sana, sasa huu ushirika ni chombo cha kumkomboa mkulima, ni chombo cha kunyanyua uchumi wa mkulima, ni chombo cha kuikomboa Rukwa, ni chombo cha kuikomboa nchi yetu ya Tanzania, nchi ambayo sasa inaelekea kwenye uchumi wa kati wa viwanda, sasa ushirika ni kitovu cha uzalishaji n ani kitovu cha viwanda, sasa kila tunachokifanya tuchote kwenye ngazi ya mkulima, lazima tujue namba moja kwenye viwanda ni uzalishaji na malighafi za kilimo zinatokana na wakulima, ni lazima azalishe na akizalisha zaidi tutakuwa na viwanda endelevu kutokana na uzalishaji mwingi” Alisisitiza
Ameongeza kuwa hali ya hewa ya mkoa wa Rukwa ni sawa na hali ya hewa za mikoa yote ya nyanda za juu kusini ambayo mikoa hiyo inaongoza kwa kulima matunda na mbogamboga na hivyo kuwa na mazao mengi mbadala kuliko kutegemea mahindi ambapo soko linaposhuka na wananchi wanakosa pa kukimbilia na hivyo kuwataka wajitafakari kutoka katika kilimo cha kutegemea mahindi na hatimae kuanza kulima mbogamboga na matunda ya kutosha kwaajili ya matumizi ya wana-Rukwa ili kupunguza udumavu pamoja na kuuza nje ya mikoa na hatimae nje ya nchi.
Mh. Wangabo ameyasema hayo katika Mkutano wa Vyama vya ushirika Mkoani humo aliouitisha ili kuwatafutia wanachama wapya chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa pamoja na kusikia mipango yao waliyojiwekea kuanzia wa mawaka mmoja hadi miaka kumi katika kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Akitoa taarifa fupi ya hali ya vyama vya ushirika Kaimu Mrajisi vyama vya Ushirika wa mkoa wa mkoa wa Rukwa Anosisye Mbetwa amesema kuwa miongoni mwa mafanikio ya mkoa ni kuanzisha chama cha kikuu cha ushirika (UCU) ambacho kimesajiliwa tarehe 9.1.2019 kikiwa na wanachama 58 na kwa ujumla hadi kufikia tarhe 31.6.2019 mkoa umeweza kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi 17,781,678,000/=.
“Vyama vya Ushirika 81 vimeweza kukaguliwa na shirika la Ukaguzi la vyama vya Ushirika nchini (COASCO) na kuhusu masoko kwa mwaka 2018/2019 soko la Serikali kwa maana ya NFRA liliwezesha upatikanaji wa shilingi 3,010,467,520/= kwaajili ya ununuzi wa mazao ya wakulima kupitia vyama vya Ushirika vya msingi,” Alisema.
Akielezea mpango wa Miaka 10 ya Chama kikuu cha Ushirika Mkoani Rukwa Makamu Mwenyekiti wa UCU Gaspar Chipeta amesema kuwa lengo kuu la chama hicho ni kuwaleta pamoja wakulima wa mkoa wa huo, kuwa na sauti moja, kutambua mahitaji ya pembejeo kwa kila mkulima kupitia vyama vya msingi pamoja na kutafuta soko lenye bei nzuri ili kuweza kuinua uchumi wa wakulima.
“Mkakati mwingi ni kuhakikisha ndani ya hii miaka kumi kuna matokeo ya uboreshwaji wa miundombinu inayotumika katika kilimo, asilimia kubwa ya wakulima katika mkoa wa Rukwa hawatumii miundombinu ya kisasa, kama ulivyosema awali kwamab lazima twende kwenye kilimo cha kisasa, sisi kama chama kikuu tunataka walau kila chama cha ushirika cha msingi, Kila AMCOS iweze kumiliki walau Trekta ambalo litaweza kuwasaidia wakulima wa vyama hivyo,” Alisema.
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya Sumbawanga Wakala wa Taifa wa Hiafadhi ya Chakula (NFRA) Abdillah Nyangasa ametahadharisha wakulima wengi wamekuwa wakilima eneo kubwa lakini mazao yanayopelekwa sokoni hayafanani na viwango na hivyo kuwataka kuzingatia ubora wa mazao katika hatua ya mwisho ambayo inapelekwa kwa mlaji, hali ambayo ipo katika mazao mengi yanayolimwa katika Mkoa.
“ Eneo la Ubora baada ya mavuno ni la msingi mno katika kupata soko zuri, wakati mwingine unaweza kuwa umevuna vizuri lakini unaleta mahindi yako sokoni utaambiwa pepeta, utaambiwa pembua mahindi yaliyooza, ondoa punji zilizoharibika na wadudu, ile ni hatua ya ziada mabayo uneifanya mwenyewe kwenye ngazi ya kaya na kwenye hatua ya chama cha msingi, tukazane kuhakikisha mazao yetu tunayaandaa vizuri kwaajili ya soko ili kupunguza gharama zisizo za lazima,” Alifafanua.
Mkoa wa Rukwa una jumla ya vyama vya Ushirika 172, kati ya hivyo 87 ni vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), 74 ni vyama vya Mazao na Masoko (AMCOS), 4 vyama vya Uvuvi, 3 vyama vya Wafugaji, 1 chama cha Wafuga Nyuki, 3 vyama vya wauza Bidhaa/huduma na Chama Kikuu cha Ushirika kimoja vyenye jumla ya wanachama 19,321.
IMG_0924 - Baadhi ya Wanachama wa vyama Mbalimbali vya Ushirika Mkoani Rukwa wakisikiliza Nasaha za Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo Pichani) katika Mkutano Ulioitishwa na Mkuu huyo wa Mkoa kwa lengo la kuwaunganisha wakulima pamoja kupitia chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa.
0 comments:
Post a Comment