Mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Makoteni Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Bimwana Saleh (12) amekufa kwa kuliwa na mamba katika mto Ligoma wakati akifua nguo na mama yake.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma, Juma Homera amemuagiza ofisa wanyamapori wa wilaya hiyo kumuua mamba huyo ili kuwanusuru wananchi na tishio la kundelea kujeruhiwa na kuuawa na mamba.
Homera amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Makoteni muda mfupi baada ya kuitembelea familia ya Mtoto Bimwana Salehe (12) aliyepoteza maisha baada ya kujeruhiwa na mamba na kutoa pole kwa wafiwa.
Aidha, Homera aliwataka wakazi wa kitongoji hicho kuchukua tahadhari na kujenga tabia ya kwenda wakiwa katika makundi wanapokwenda kuchota maji au kufua katika mto huo.
Alisema utaratibu wa kwenda watu wengi kwa pamoja mtoni utawasaidia kuokoana endapo ikitokea mmoja wao kuvamiwa.
Homera aliwataka wazazi na walezi katika kata hiyo kuacha taratibu za kuwatuma watoto wadogo kwenda kufanya shughuli zozote katika mto huo.
Mtendaji wa kijiji cha makoteni Ajili Mbemba alimueleza mkuu wa wilaya kuwa watu wawili wamekwishapoteza maisha na wengine watano walijeruhiwa kwa kushambuliwa na mamba katika eneo hilo katika kipindi cha Julai 2018 hadi Februari mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mbemba waliopoteza maisha ni Furaha Mtindinganya (15) aliyekufa mwanzo mwa mwezi Januari mwaka huu na Bimwana Hashim aliyepoteza maisha Februari 26 mwaka huu.
Aidha Mbemba aliwataja waliojeruhiwa na mamba hao na kusababishiwa vilema vya maisha katika eneo la mto huo kuwa ni Shabilu Mohammed (8), Muhdini Dhabiti(29), Katrimu Juma (11), Saidi Issa (19) na merina Omari (15).
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa kata hiyo Abbas Ngajime walioomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapunguza mamba hao ili wananchi waweze kuishi kwa amani.
Akizungumzia hali hiyo Kaimu Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya Tunduru Limbega Ali pamoja na kukiri kuwepo kwa matukio hayo alisema kuwa tayari amekwishatuma askari wenye silaha kwa ajili ya kwenda kumsaka na kumuua mamba huyo ili asiendelee kuleta madhara kwa watu.
0 comments:
Post a Comment