Wananchi Waonywa wengine wakamatwa baada ya kuishambulia gari ya Serikali - Rukwa.


IMG_8334 - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (katikati) akitoa maelekezo kwa meneja wa pori la Akiba la Uwanda Jovine Nachihangu (kulia) juu ya kuhakikisha alama zinazowekwa kwenye mipaka ya hifadhi hiyo inakuwa na maandishi yanayoosomeka kuwa unaingia katika hifadhi ili kupunguza migogoro na wananchi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt Khalfan Haule.  

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaonya wananchi wa Kijiji cha Nankanga, Kata ya Nankanga, Wilayani Sumbawanga kuacha tabia ya kuharibu mali za serikali ili kutafuta suluhu ya migogoro iliyopo baina yao na askari wa hifadhi ya Pori la Akiba Uwanda katika bonde la ziwa Rukwa huku akimuagiza kamanda wa polisi Mkoa kuwasaka na kuwakama wote waliohusika na uharibifu huo.
Ametoa maagizo hayo baada ya gari ya hifadhi hiyo kushambuliwa na wavuvi waishio katika kambi ya uvuvi ya Kijiji cha Nankanga kilichopo pembezoni mwa ziwa Rukwa, tukio lililotokea tarehe 10.4.2019 ambapo wavuvi hao walivunja vioo vya gari, kuchomoa tairi pamoja na kuchukua vitu vilivyokuwamo ndani ya gari huku dereva wa gari hiyo kukimbia na kuicha gari hiyo.
Alisisitiza kuwa wananchi hawawezi kufanya uhalifu ili kuhalalisha madai yao na  uhalifu haulipwi kwa uhalifu na kuongeza kuwa mahali popote penye uhalifu, sheria huchukua mkondo wake, sio kuanza uharibifu na vitendo vingine vya uvunjifu wa amani mpaka kutishia uhai wa watu hivyo aliwataka wana Nankanga kujitafakari kwa kina na kujitambua.
“Hebu fikiria hiyo gari kama ingechomwa moto na uvunjifu mwingine wa amani mkubwa ungetokea mnadhani mngelala kwenye Kijiji chenu hiki, wengine mngetumbukia kwenye maji, wengine mngepanda mlima bila ya kujua na wengine msingekaa kurudi hapa, kwahiyo mimi ninawaonya na ninawakanya iwe ni mara ya kwanza na ya mwisho, ninyi kama wanakijiji kuleta uvunjifu wa amani ndani ya Kijiji, msije mkagusa tena mali ya serikali, bahati mbaya sikujua gharama za uharibifu mlioufanya mngechanga Kijiji kizima kulipa huo uharibifu ambao mmeshaufanya,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Meneja wa Pori la Akiba la Uwanda Jovine Nachihangu alisema kuwa mgogoro huo ulitokana na askari wa hifadhi hiyo kukamata mitumbwi sita na wavuvi 18 waliokuwa wakivua katika eneo la hifadhi ndani ya ziwa Rukwa ambapo hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 5000 huku eneo la nchi kavu likiwa na kilomita za mraba 490.
“Wakati nipo Mbeya, nilipokea simu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya kwamba kuna watu wanataka kuvamia kambini kwahiyo nichukue tahadhari, kwahiyo nilianza kuwasiliana na watu waliomo humu kuwa kuna jambo hili na hili linataka kutokea, gari ilipata pancha Kijiji kwasababu tunakawaida ya kumchukua mwenyekiti wa Kijiji ili kuwatambua watu wake lakini muda huo dereva alinipigia simu kunambia hali siyo nzuri na ameiacha gari kijijini, hivyo tuliwasiliana na polisi ili kuomba msaada,” Alieleza.
Wakati akifafanua tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alisema kuwa mahusiano baina ya wananchi na askari wa hifadhi hiyo sio mazuri lakini kitendo cha wananchi kuvamia gari ya serikali kuipiga mawe na kuiba hakifai na kuongeza kuwa hifadhi hiyo ina mipaka ya muda na mipaka ya kudumu bado infanyiwa tathmini na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala.
“Waziri Kigwangala mwaka jana alikuwa hapa na miongoni mwa matatizo tuliyomueleza ni mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi na wavuvi, nchi kavu huku tunashukuru alama zimewekwa na zimepunguza migogoro iliyopo kati ya wananchi na hifadhi, bado tuna changamoto ya mifugo nae neo la wavuvi bado wavuvi wanaingia hifadhini,” Alisema.
Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Nankanga Anyisile Kayuni alisema kuwa tukio lililotokea limetokana na chuki kati ya wavuvi na wahifadhi na kudai kuwa wavuvi wanahisi wanaonewa wakati wahifadhi wanatekeleza majukumu yao ya kisheria.
“Mgogoro huu nimeukuta tangu naingia udiwani umepitia hatu anyingi sana hadi kufikia Waziri Dkt. Kigwangala kuwasimamisha watumishi 27 wa wanayapori lakini mgogorio huu bado haujaisha, Mh. Mkuu wa Mkoa wakazi hawa wa Nankanga wamepungua idadi uliyoikuta wakati ule wa masika sio hii asilimia kubwa wamekimbilia forodha ya masuche jirani hapo (wilaya ya) Momba (Mkoani Songwe) wakitokea mwalo huu hapa,” Alieleza.
Katika hatua nyingine Mh. Wangabo aliwatahadharisha askari wa wanayamapori kutotumia sheria vibaya na hatimae kuwaonea wananchi kwa kuwapiga bila ya mpangilio na huku akiwataka wananchi hao kuhakikisha wanatii sheria na inapotokea wanakiuka sheria hizo basi waache ubishi wakati wanapokamatwa.
Katika kipindi cha mwezi Novemba mwaka 2018 hadi Machi 2019, Wanyama walioonekana katika pori hilo la Akiba la Uwanda lililopo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Wanyama walioonekana ni Nyati, Swala, Fisi na Tembo.
Share on Google Plus

About KAPOLA NEWZ TV..✍️

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment