Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali imeona umuhimu wa kuingiza elimu ya mlipa kodi kwenye mitaala ya elimu nchini ili kwajengea Watanzania tabia, mwenendo na mazoea ya kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa jana, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Lupembe Mhe. Joram Ismael Hongoli juu ya kwa nini Serikali isiingize kwenye mitaala ya elimu somo la umuhimu wa kulipa kodi ili lifundishwe kuanzia shule ya msingi ili wananchi wapate uelewa wa kodi na waweze kulipa kodi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea.
“Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya mlipa kodi katika kumjengea mwananchi tabia ya kulipa kodi. Katika somo la Uraia na Maadili kuanzia darasa la III na kuendelea, mtaala umelenga kumjengea na kumuandaa mwanafunzi kuwa mwajibikaji katika kutekeleza majukumu ya kila siku,” alisema Mhe. Ole Nasha.
Vile vile mtaala umelenga kumjengea mwanafunzi kuiheshimu na kuithamini jamii yake kwa kuwa mwadilifu na mzalendo ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu ya kitaifa ikiwemo kulipa kodi.
Aidha amesema, kutokana na umuhimu wa kuwajengea vijana utamaduni wa kulipa kodi, elimu ya mlipa kodi ni jambo muhimu, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikisha Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) itaendelea kuboresha elimu hiyo ili isisitizwe na kuwekewa mkazo katika mitaala ya elimu kuanzia elimu ya Msingi.
Wakati huo huo, Mhe. Ole Nasha amesema Serikali ilifuta ada na michango ya lazima katika shule za umma ngazi ya elimu ya msingi (elimu ya awali hadi kidato cha Nne) na mpango huo hakuhusisha kidato cha tano na sita pamoja na shule binafsi.
Ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Seter Alexander Mahawe juu ya lini, Serikali itafuta ada kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi.
“Ada na michango iliyokuwa inalipwa na wazazi/walezi kwa sasa hugharamiwa na Serikali. Mpango huu haukuzihusu shule binafsi pamoja na shule za Umma ngazi ya kidato cha Tano na Sita. Hivyo shule hizo zitaendelea na utaratibu wa wazazi/walezi kuchangia gharama za uendeshaji wa elimu ikiwemo kulipa ada za mitihani.
Hata hivyo amesema, Ili kuhakikisha mazingira rafiki katika utoaji wa elimu, Serikali imekuwa ikifanya majadiliano na sekta binafsi kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili ambapo hadi sasa Serikali imeweza kuondoa baadhi ya kodi na tozo mbalimbali ambazo awali walikuwa wakitozwa wamiliki wa shule binafsi.
Ametoa mfano wa kodi hizo kuwa ni kodi za mabango, kodi ya kuendeleza ufundi standi stadi (Skills Developmentt Levy), tozo ya Afya na Usalama mahala pa kazi (Occupational Safety and Health Administration – OSHA) na tozo ya zimamoto.
0 comments:
Post a Comment