Wachungaji watatu wamenusurika kipigo kutoka kwa wananchi, baada ya kushindwa kumfufua marehemu katika Kijiji cha Sitalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.
Wachungaji hao walifika kijijini hapo wakidai kuwa wanao uwezo wa kumfufua marehemu mwanakijiji mwenzao aliyefariki dunia hivi karibuni na kuzikwa kwenye makaburi ya Kijiji hicho.
Akisimulia tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Angelo, alisema kuwa tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi lilitokea Mei 7, majira ya saa 4 za asubuhi kijijini hapo.
Alisema kuwa wachungaji hao ambao walikuwa watatu walifika kwenye ofisi ya Kijiji na kujitambulisha kuwa wao ni wachungaji wanatoka katika Kijiji cha Nsimbo na watakuwapo kijijini hapo wakiwa wameitwa na ndugu wa marehemu, Raymond Mirambo aliyefariki dunia siku moja na kuzikwa kijijini hapo.
Alisema wachungaji hao walifika kijijini hapo wakidai kuwa wanataka kufanya maajabu ambayo ni ya kihistoria nchini ya kufanya maombi mfululizo na kumfufua marehemu Raymond.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na kujitambulisha kwa wachungaji hao kwenye ofisi ya kijiji, uongozi wa kijiji uliwaruhusu wachungaji hao kufanya maombi hayo ya kumfufua marehemu huyo.
Alisema baada ya kuruhusiwa na uongozi wa kijiji walielekea nyumbani kwa marehemu na kuwakuta ndugu wakiwa wanawasubiri kwa ajili ya maombi hayo ya kumfufua ndugu yao.
Alisema maombi hayo yaliendelea kwa muda wa siku saba usiku na mchana pasipo kuwa na mafanikio yoyote, hali ambayo iliwafanya ndugu wa marehemu washikwe na hasira.
“Wananchi, ndugu na jamaa walikasirika kutokana na kuona kuwa wachungaji hao wanawatapeli na kwa sababu waliwasababishia kuingia gharama kubwa ya kulisha watu waliokuwa wakishiriki maombi hayo,” alisema.
Kwa mujibu wa Angelo, baada ya kuona hafufuki, ndugu wakiongozwa na mama mzazi wa marehemu waliamua kwenda kutoa taarifa ofisi ya kijiji, ili kuepusha vurugu ambazo zilitaka kutokea.
Alisema watu walioonekana kuwa na hasira kwa kutoona muujiza wa kumfufuka marehemu walitaka kuwapiga wachungaji hao kwa kuwapotezea muda na kuwatapeli.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa Kijiji baada ya kufika kwenye eneo hilo walikuta ndugu wa marehemu wakiwa wanafoka kwa hasira huku wakiwa wanawatuhumu wachungaji hao kuwa ni matapeli.
“Sisi uongozi wa Kijiji tulikuta vurugu na wananchi walikuwa wanataka kuwapiga wachungaji hao, tulichofanya kuepusha shari ni kuwaondoa wachungaji hao eneo hilo na kwa kweli walitii agizo hilo na kuondoka zao,” alisema Angelo.
0 comments:
Post a Comment