Kamanda wa Polisi Mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo
**
Mtu mmoja kati ya wanne waliokamatwa katika operesheni ya kudhibiti uvuvi haramu Ziwa Victoria, amefariki dunia kutokana na kile kinachodaiwa kuwa alipata kipigo kutoka kwa askari wanaosimamia operesheni hiyo.
Aliyefariki dunia ni Paschal Kanyembe (40), mkazi wa Kitongoji cha Mlila, Kijiji cha Rubambangwe wilayani Chato mkoani Geita.
Mbali na Kanyembe, watuhumiwa wengine waliokamatwa na kudaiwa kujeruhiwa katika operesheni hiyo ni Busu James, Emmanuel Luchagula na Rusato Magesa.
Akizungumzia tukio hilo, mke wa marehemu, Ester Justine (39), alisema juzi kuwa majira ya saa saba usiku wa kuamkia Jumanne, askari wa doria ya kudhibiti uvuvi haramu walifika nyumbani kwake na kutoa amri kwa wanandoa hao kufungua mlango.
Alisema walilazimika kuomba dakika chache ili wavae na askari hao walikubali na kuwapatia dakika mbili za kufanya hivyo na baadaye wanandoa hao walifungua mlango wa nyumba yao.
Ester aliendelea kueleza kuwa, pasi na kujua kinachoendelea, askari wawili kati ya kundi kubwa lililokuwa nyumbani kwake, waliingia ndani na kumweka chini ya ulinzi mume wake huku wakimtaka kusalimisha nyavu haramu walizodai amezificha.
"Baada ya mume wangu kuwaambia kuwa hausiki na uvuvi wa aina yoyote ile, walianza kumshambulia kwa marungu na mateke huku wakimvuta kwenda nje," Ester alieleza.
"Hata walipomfikisha nje waliendelea kumpiga sana hadi akashindwa hata kukaa chini, akabaki amelala chali.
"Nikiwa mlangoni, nilishuhudia kipigo hicho, lakini baadaye askari waliniamuru kurudi ndani kulala huku wakiondoka na mume pamoja na vijana wengine watatu ambao tayari walikuwa wameshawekwa chini ya ulinzi.
"Majira ya saa mbili asubuhi leo (Jumanne) nilipiga simu ya mume wangu ili kujua kama ameachiwa lakini ilipokelewa na mmoja wa askari hao ambaye alianza kuniuliza kama mume wangu huwa ana ugonjwa wa kifafa, kisukari au shinikizo la damu.
"Nilipowajibu kuwa hajawahi kuugua magonjwa hayo, wakaniambia 'tafuta usafiri uje kwa mume wako yupo huku Kituo cha Afya cha Nyabugera Muganza'. Ikabidi niende huko."
Ester aliongeza kuwa mume wake alipelekwa katika kituo hicho na askari hao.Rafiki wa marehemu, Didas Emmanuel, alisema juzi kuwa baada ya kufika Kituo cha Afya Muganza akiwa na Ester, alishuhudia rafiki yake akiwa hajiwezi huku akiwa anaongezwa maji mwilini kwa sindano.
Alisema kuwa matabibu waliokuwa wanampa kituoni hapo, walimshauri kwenda kituo cha polisi kuchukua fomu ya polisi ya kuruhusu mtu aliyejeruhiwa kutibiwa (PF3) kabla ya mgonjwa wao kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa ajili ya matibabu zaidi.
"Tukiwa njiani kwenda hospitali ya wilaya kumwahisha mgonjwa wetu ili apatiwe matibabu, majira ya saa 5:30 asubuhi, ndugu yetu alikata roho," alisema.
Wakazi wengine wa eneo hilo, Daud Kingu na Enos Petro, walidai vitendo vya askari wa doria ya uvuvi haramu kupiga wananchi ovyo, kuvamia nyumba za watu usiku, kupora simu na fedha za wananchi vimekuwa vikitokea mara kwa mara kwenye maeneo yao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk. Eligobeth Kalisa, alikiri kupokea maiti ya mtu huyo pamoja na wagonjwa wengine watatu waliopelekwa na Idara ya Maliasili ambao walitibiwa na baadhi yao kuruhusiwa kuondoka baada ya afya zao kuimarika.
"Itoshe tu kusema kuwa taarifa za uchunguzi (Kanyembe) tumeshawapatia polisi. Na unajua mambo haya yakishakuwa kwenye jinai, sisi haturuhusiwi kuyazungumzia. Kwa hiyo, mambo mengine watafute polisi," alisema Dk. Kalisa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa kifo hicho kilitokea kwa bahati mbaya kwa kuwa lengo la askari hao ni kudhibiti uvuvi haramu na siyo vingine.
"Ni kweli tukio hilo lipo na umauti ulimkuta kijana huyo jana (juzi) majira ya saa sita mchana akiwa amefikishwa kwenye Kijiji cha Mkuyuni wakati akiwahishwa hospitali kwa matibabu zaidi baada ya kumpatia rufani kutoka Kituo cha Afya cha Nyabugera. Kijana huyo alipungukiwa nguvu na umauti kumkumba," alisema Mwabulambo.
0 comments:
Post a Comment