Watu huwa na imani tofauti na huabudu vitu vingi duniani. Nchini Nigeria, kuna kabila moja ambalo humuabudu mamba kama miungu.
Mamba huyo wanayemuabudu kwa sasa ana umri wa miaka 78.
Wakazi wa eneo hilo la Oje viungani mwa mji wa Ibadan kusini magharibi mwa Nigeria humuenzi mamba huyo sana na wanaamini kwamba mamba huyo anaweza kujibu maombi yao.
Huwa wanamrushia kuku kama zawadi kumshawishi kutimiza maombi yao, wengine humpa mbuzi.
Mamba huyo humilikiwa na familia ya Delesolu ambao wamekuwa wakimfuga kama mnyama kipenzi. Anadaiwa kuanza kufugwa na familia hiyo kuanzia mwaka 1940 baada ya mamba mwingine aliyekuwa akifugwa kabla yake kuchukuliwa na Wazungu.
Ajabu ni kwamba familia hiyo yenyewe huwa haiamini kwamba ana nguvu zozote za kipekee.
Kiongozi wa sasa wa familia hiyo ya Delesolu, Bw Raufu Yesufu, aliambia BBC kwamba: "Kwa sababu ya Imani yetu, sisi ni Waislamu, hatuamini kwamba ana nguvu zozote."
Lakini hilo huwa haliwazuii watu kuendelea na imani zao.
Anasema waganga wa kienyeji na matabibu wengine huwa wanafika kwa sababu mbalimbali kutafuta msaada.
Baadhi hufika kuomba usaidizi katika kuwaponya wagonjwa au kuwasaidia watu wanaotatizika kushika mimba.
Familia hiyo huwa haiwazuii kufika kumuomba mamba huyo ambapo huwa wanampa kuku.
Watu wamekuwa wakifika kwa mamba huyo kwa muda mrefu, baadhi wakiwa na maombi ya ajabu.
Kunao wanaofika wakitaka kuchukua kinyesi chake na wengine kutaka kuchotamaji kutoka kwa kidimbwi anamoishi.
Bw Yesufu anasema kinyesi hiyo na maji hayo baadaye hutumiwa na waganga au watu binafsi kama tiba.
Chanzo-BBC
0 comments:
Post a Comment