Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jakaya Kikwete amewataka wahitimu wa shahada za ualimu kujiandaa kisaikolojia kufundisha shule za msingi badala ya shule za sekondari kama yalivyo matarajio yao.
Ameyasema hayo kwenye mahafali ya 10 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam cha Elimu Mkwawa cha mjini Iringa baada ya kutunuku Shahada za kawaida kwa wahitimu 1,340 na Stashahada ya Uzamili kwa wahitimu sita.
“Serikali sasa inapeleka wanafunzi wenye shahada kufundisha shule za msingi, jambo hili halikupokewa vizuri na wale wa mwanzo, waliona kama wanashushwa hadhi kwa sababu stahili yenu ni kufundisha sekondari,” alisema na kuongeza kuwa maamuzi hayo ya Serikali ni sehemu ya mapinduzi makubwa ya elimu yanayoendelea kutokea nchini na kwa mazingira ya sasa hayaeupikiki.
“Tulikuwa na walimu wa shule za msingi waliokuwa wahitimu wa darasa la saba na la nane, leo hawapo sasa tuna wa daraja la tatu A ambao ni wa kidato cha nne ambao nao watapotea kwa sababu ya ongezeko la walimu wa Diploma na Shahada,” alisema.
Akizungumzia mapinduzi ya elimu katika nchi zilizoendelea, Kikwete alisema walimu wanaofundisha kuanzia chekechea hadi sekondari katika nchi hizo ni wale wenye elimu ya chuo kikuu.
Kutokana na mabadiliko hayo amesema uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umeanza kuangalia namna utakavyobadili mitaala yake ili wahitimu wa shahada za ualimu katika vyuo vyake waweze kumudu kufundisha wanafunzi wa ngazi ya msingi hadi sekondari.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye aliwataka wahitimu hao kutumia elimu yao kuikomboa jamii badala ya kuibomoa.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema baraza linaendelea kushirikiana na wadau kuimarisha chuo na kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali.
Katika hotuba yao iliyosomwa na mhitimu aliyefanya vizuri kuliko wanafunzi wote, Emanuel Kayuni, wahitimu hao waliwaasa wanafunzi wenzao wanaobaki chuoni hapo kujituma katika masomo yao, kudumisha umoja, nidhamu, hekima na mshikamano.
0 comments:
Post a Comment