Watoto wanne wa familia moja wamefariki dunia kwa kuteketea kwa moto walipokuwa wamelala chumbani katika tukio lililotokea mtaa wa Geita Road Kata ya Nyatukala mjini Sengerema mkoani Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amesema tukio hilo lilitokea saa tano usiku wa Februari 28, 2018 na kuwataja watoto hao kuwa ni Redia Elias (10), Modesta Elias (9), Steven Deogratias (9), na Kizengela Elias mwenye umri wa miaka ninane.
Amesema wakati moto huo uliotokana na mshumaa kushika chandarua na kuunguza godoro walilokuwa wamelalia, mama yao alikuwa amelala kwenye nyumba nyingine ya familia hiyo.
“Watoto wote ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Pambalu na wanatarajiwa kuzikwa kesho,” amesema Kipole.
Mmoja wa majirani wa familia hiyo, Amas Juma amewataka wazazi kuwa makini pale wanapolazimika kuwawashia watoto mishumaa kwa kuhakikisha inazimwa kabla ya kulala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na kutoa wito kwa wazazi na walezi kuchukua tahadhari watoto wanapobaki wenyewe nyumbani.
0 comments:
Post a Comment