MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewahukumu watu watatu akiwamo aliyekuwa Sajenti George Kwisema wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kwenda jela miaka 40 baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha na kukutwa na vipande 10 vya meno ya tembo yenye thamani ya Sh. milioni 198.
Mbali na Sajenti Kwisema, washtakiwa wengine waliosomewa hukumu hiyo na Hakimu Mkazi Mkuu Respius Mwijage ni Nia Bakari na Shafii Muhibu.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilimwachia mshtakiwa wa pili, Asha Ulaya, baada ya ushahidi uliotolewa kushindwa kuthibitisha kosa dhidi yake.
Hakimu Mwijage alisema baada ya kupitia ushahidi wa Jamhuri, mahakama yake bila kuacha shaka imewatia hatiani mshtakiwa wa kwanza, wa tatu na wa nne.
"Washtakiwa mtakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 20 kwa kosa la kwanza, pia mtakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mingine 20 kwa kosa la pili lakini adhabu yenu itakwenda sambamba. Meno ya tembo na gari aina ya Suzuki Escudo vinataifishwa na serikali,"alisema Hakimu Mwijage wakati akisoma hukumu hiyo.
Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Elia Athanas, ulidai kuwa washtakiwa wapewe adhabu kali ili iwe fundisho.
"Mheshimiwa washtakiwa wanastahili adhabu kali hasa mshtakiwa wa kwanza kwa kuvunja kiapo cha kulilinda taifa lake kama askari wa JWTZ " alidai Athanas.
Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadaiwa Juni 2, 2016 walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vikiwa na thamani ya Sh. 198,000,000 mali ya serikali ya Tanzania.
0 comments:
Post a Comment