Serikali ya Tanzania imekanusha tuhuma kwamba inaminya demokrasia nchini humo na kusema kuwa imesikitishwa na matamko kadhaa yaliotolewa na Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) na kuungwa mkono na baadhi ya balozi za nchi za Magharibi.
Taarifa ya serikalli ya Tanzania imefuatia matamko yaliyotolewa na nchi za magharibi wiki za hivi karibuni yakielezea wasiwasi wao kutokana na matukio ya kiusalama ambayo wameeleza yanatishia utawala wa kisheria na maadili ya kidemokrasia nchini Tanzania.
Katika wiki za hivi karibuni polisi wa Tanzania wameshutumiwa kwa kutumia nguvu za kupita kiasi kushughulikia mivutano ya kisiasa na pia wanasiasa kadha wa upinzani wakiwemo wabunge mara kwa mara wameitwa polisi kwa mahojiano kutokana na madai ya kufanya mikutano isiyo halali.
Mbunge wa upinzani Joseph 'Sugu" Mbilinyi na afisa mwingine wa chama cha Chadema mjini Mbeya walihukumiwa kifungo cha miezi mitano gerezani mwishoni wa Februari baada ya kukutwa na hatia ya kumkashifu Rais John Pombe Magufulu
Taarifa hiyo iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania pia imesema kuwa tayari nchi hiyo imechukua hatua kukubaliana na vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini. Nchi za magharibi ziliishutumu Tanzania kwa kukiuka vikwazo hivyo.
Hata hivyo Tanzania imesema tuhuma kwamba imekiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na programu yao ya makombora ya balistika hazijaweza kuthibitishwa..
Taarifa hiyo imeeleza kuwa suala la utawala wa sheria na demokrasia katika tamko hilo la mabalozi linaonyesha sintofahamu iliyoko juu ya usalama na changamoto za kisiasa ambazo Tanzania imekuwa ikikabiliwa nazo kwa kipindi cha miezi 18 na kwamba matamko hayo yamekuwa sio tafsiri sahihi ya hali ya kisiasa na usalama iliyopo Tanzania.
“Ni kawaida kwa wanadiplomasia wa kigeni kufuatilia na kuripoti hali ya kisiasa na usalama inayoendelea katika nchi walizotumwa. Lakini tunashangazwa na ukimya uliowazi katika kipindi cha nyuma wa mabalozi hawa juu ya vitisho vya uvunjifu wa amani uliokuwa haujawahi kutokea na changamoto nyingine ambazo Tanzania imekuwa ikikabiliana nazo katika maeneo matatu ya Kibiti-Mkuranga –Rufiji yanayopakana,” limesema tamko hilo.
Wizara hiyo imeeleza kuwa vitisho hivyo vimewauwa watu wasio na hatia na kwa sadfa ya ajabu, wengi wa waliouwawa walikuwa kutoka chama tawala.
Mauaji hayo yalikuwa yametanguliwa na matukio kama hayo ya uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ya nchi yakiwa ya aina yake yalihusisha uvunjifu wa amani.
Kwa mujibu wa tamko hilo pamoja na kuwepo taarifa za matukio haya ya uvunjifu wa amani yalitolewa na vyombo vya habari nchini, hakukuwa hata na tamko lililolaani vitendo hivyo kutoka kwa mabalozi hao.
Wizara imehoji kuwa ni hivi sasa tu ndio EU inataja juu juu shambulizi la silaha lililotokea Mkoa wa Pwani katika kipindi cha miaka miwili.” Kuchelewa kutolewa kwa matamko hayo baada ya muda mrefu na wakati mgumu unastaajabisha.
Moja ya matamko yaliyotolewa na mabalozi wizara imesema ni jambo zuri kwa mabalozi wametambua wito wa Rais Magufuli akitaka uchunguzi ufanyike wa matukio mengine ya uvunjifu wa amani katika wimbi la operesheni ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji.
Lakini wizara imesema kuwa matamko hayo ya mabalozi hayakutambua uhusiano uliokuwepo kati ya hatua za kishujaa ambazo zimechukuliwa na Rais Magufuli kuondoa ufisadi, madawa ya kulevya, ukwepaji kodi, ujangili wa nyara za serikali na kuhakikisha uwajibikaji katika sekta binafsi na za umma, na matukio ya usalama.
0 comments:
Post a Comment