MKAZI wa Mrito, kata ya Kemambo Nyamongo
aliyefahamika kwa jina Chacha Magige (30) amehukumiwa adhabu ya
kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa
kumkatakata kwa panga sehemu mbalimbali Mackrina Isaya.
Mtuhumiwa huyo alimkata Mackrina mikono yote miwili hadi kukatika kabisa na kusababisha kifo chake.
Akisomewa hukumu hiyo katika kesi ya
mauaji Mahakama Kuu yenye namba 181/2 /2017, Mei 5, mwaka huu katika
kikao cha Mahakama Kuu kinachoendelea katika Mahakama wilayani ya Tarime
mkoani Mara Jaji wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza, Joaquine De- Mello
alidai kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka
ukiongozwa na mwanasheria wa serikali, Harry Mbogoro.
Mwanasheria huyo wa serikali alidai kuwa
mtuhumiwa Chacha Magige alitenda kosa hilo Julai 2, mwaka 2011 asubuhi
katika Kijiji cha Mrito kwa kumshambulia kwa kumkatakata kwa panga
Mackrina, mikono yote miwili na kukatika, alimshambulia kichwani na
kumsababisha kifo, baada ya kumnyang’anya mwanamke huyo simu yake ya
mkononi na Sh 1,000,000.
Katika mashitaka hayo mtuhumiwa alikiri
kumuua mwanamke huyo na kudai kuwa ilikuwa ni hasira za kumdai shilingi
10,000,000 alizodai alimpa amhifadhie na kwamba walikuwa na mahusiano ya
karibu na Mackrian na kuiomba mahakama hiyo kumuadhibu kwa kuua bila
kukusudia.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Serikali
Mbogoro alipinga utetezi huo na kudai kuwa mtuhumiwa alikuwa na nia ya
kuua kwani Mackrina alikutwa na majeraha manne makubwa ya kukatwa mikono
yote miwili, jeraha kubwa ubavuni na kichwani.
Jaji Joaquine akitoa hukumu alikubaliana
na maelezo ya mwanasheria wa serikali na kumtia hatiani kwa kosa la
kuua kwa kukusudia. Mtuhumiwa baada ya hukumu hiyo aliomba maji ya
kunywa.
0 comments:
Post a Comment