Basi la shule ya msingi Little Treasures iliyopo katika manispaa ya Shinyanga imepata ajali na kupinduka na kutumbukia mtaroni eneo la Kalogo mjini Shinyanga na kusababisha majeraha kwa wanafunzi kadhaa.
Ajali hiyo imetokea leo Alhamis Januari 10,2019 majira ya saa tisa alasiri wakati basi hilo lenye namba za usajili T183 AFE likitoka shuleni eneo la Bugayambelele kata ya Kizumbi kuelekea Ushirika likirudisha wanafunzi majumbani.
Akizungumza na Kapola newz, Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Simon Haule amesema hakuna madhara makubwa yaliyotokea bali baadhi ya wanafunzi wamepata majeraha madogo madogo.
Amesema basi hilo lilikuwa limebeba wanafunzi 30 na tayari waliojeruhiwa wamepatiwa matibabu kati yao wanne bado wapo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
"Basi lilikuwa linatoka shuleni likipeleka wanafunzi/watoto majumbani mwao,lilipofika eneo la Kalogo karibu na ofisi za TANROADS likapinduka na kusababisha majeraha kwa wanafunzi ambao wamekimbizwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga ambapo baadhi wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kutoka ,wanne bado wanapatiwa matibabu",amesema Kamanda Haule .
Kamanda Haule amekitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni dereva wa gari hilo kuendesha huku akichezea simu/akichat na baada ya ajali kutokea alikimbia na wanaendelea kumtafuta.
Muonekano wa gari la shule ya Little Treasures baada ya kupata ajali
0 comments:
Post a Comment