Majengo ya Maabara na madarasa yanayotakiwa kumaliziwa ili shule ya Sekondari Ntapepa iweze kusajiliwa na wananfunzi waanze kusoma
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akihamasisha uchangiaji wa fedha na vifaa katika kuhakikisha Shule ya Sekondari Ntatepa inakamilika na kusajiliwa mwaka huu 2019.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Myula, Wilayani Nkasi walioshiriki kwenye Harambee ya kuchangia umaliziaji wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Ntatepa.
Picha ya pamoja kati ya Wananchi wa Kata ya Ntapepa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo mara tu baada ya kufanya harambee ili kuhakikisha shule ya Sekondari Ntapepa, Kata ya Myula, Wilayani Nkasi.
Majengo ya madarasa yanayotakiwa kukarabatiwa ili shule ya Sekondari Ntapepa iweze kuanza, madarasa hayo yameanza kujengwa tangu mwaka 2008.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuhakikisha Shule ya Sekondari ya Ntatepa iliyopo kata ya Myula, Wilayani Nkasi inasajiliwa mwezi wa tatu mwaka 2019 ili kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao watahamishwa kutoka shule za kata za jirani na hatimae kuwapunguzia umbali wa kutembea wanafunzi wanaotoka katika kata hiyo kwenda kata za jirani kusoma.
Amesema kuwa ili kuhakikisha kasi ya ujenzi wa shule hiyo inaongezeka atachangia bati 100 na kuwataka viongozi wote wa serikali za vijiji vitano vinavyounda kata hiyo vyenye kaya 2547 kuhakikisha kila kaya inachangia shilingi 5000 ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ambao ulianza mwaka 2008 na kuwekwa jiwe la msingi mwaka 2013 na aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Aggrey Mwanri.
“Mimi inaniuma sana kuona tangu mwaka 2008 hii shule, haijaanza, haijasajiliwa, lile jengo pale la waalimu nimesoma pale lile jiwe la msingi liliwekwa na Mh. Mwanri wakati huo akiwa Naibu Waziri TAMISEMI mwaka 2013 leo hii ni mkuu wa Mkoa wa Tabora, najisikia vibaya, miaka mingi 11 shule haianzi, basi na ianze mwaka huu, nitumie nafasi hii kuwahamasisha wanakata wote wa Myula, tuchangie shule imlizike,” Alisema.
Aliyasema hayo tarehe 11.1.2019, alipotembelea shule hiyo ili kubaini mkwamo uliopelekea shule hiyo kushindwa kusajiliwa na kuweza kusomesha wanafunzi, Aidha Mh. Wangabo alirudi tena tarehe 22.1.2019 kufanya harambee ili kupata fedha za kufanya ukarabati wa madarasa manne ya wanafunzi, nyumba ya mwalimu mkuu ambayo ilikuwa tayari pamoja na kumalizia madara mawili na maabara ambayo ilikuwa ndio kikwazo cha kusajiliwa kwa shule hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Nkasi Kusini Mh. Desderius Mipata alisema kuwa shule ambazo walitakiwa kufungua pamoja na shule hiyo tayari zimeshaanza kutoa wanafunzi wa kidato cha nne na baada ya kuona kuwa mwaka huu ufaulu umeongezeka ndipo alipoushirikisha uongozi wa wilaya ili kuona namna ya kukabiliana na vikwazo vinavyoifanya shule hiyo isisajiliwe ili waweze kuvikamilisha.
“Hatujafanikiwa hapa kwasababu viliongezeka vigezo vya kufanya shule isifunguliwe lakini pia na mkazo wa kusaidia, mwaka huu baada ya kuona ongezeko kubwa sana la ufaulu na upungufu wa madarasa tulikaa na Mh. Mkuu wa Wilaya tukatembelea hapa na kuhamasisha vijiji vyote kufanya songambele na kuwezesha kuendeleza miundombinu hii, madarsa mawili na maabara moja ili iwe ni vya kuanzia,” Alisema.
Wakati akielezea sababu za kushindwa kusajiliwa kwa shule hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Missana Kwangura alisema kuwa uchache wa wanafunzi ulikwamisha kusajiliwa kwa shule hiyo pamoja na kutokuwepo kwa maabara lakini sasa wanafunzi ni wengi mno hivyo ni kuamilisha maabara tu ndio kutapelekea shule hiyo kusajiliwa na kuongeza kuwa shule hiyo inaweza kuanza kama shule shikizi ya shule ya sekondari Kate ambayo ni kata ya jirani wakati taratibu za usajili zikiendelea.
“Mh. Mkuu wa Mkoa tutapambana mwaka huu ili walau shule hii iweze kuanza mwaka huu hata kama kuwa shule shikizi ya shule mama ya Sekondari ya Kate, kata hii pia ina vijiji vitano kama ilivyo kata ya Kate, tuombe tu kushirikiana wote na wananchi na ushauri ambao umeutoa walau wa kutumia eneo hili vizuri, tutahakikisha hii shule walau inaweza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na hata waalimu wachache wa kuanzia,” Alimalizia.
Katika harambee iliyoendeshwa na Mh. Wangabo ii kumalizia shule hiyo zilipatikana shilingi milioni 6.9, mifuko ya saruji 240, mbao za kupaulia 200, maguni ya mahindi 3, gunia 1 la maharage, mbuzi 1, kondoo 1, na kuku pamoja na gunia 2 za mbegu za maharage kwaajili ya kilimo hicho katika eneo la shule lenye ukubwa wa ekari 100. Michango yote ikiwa ni ahadi pamoja na mawasilisho.
0 comments:
Post a Comment