Bango la ramani ya Viwanja vya Kanondo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga James Mtalitinya akionyesha ramani ya viwanja vilivyotengwa kwaajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo na maghala katika eneo la Kanondo, kata ya Ntendo Manispaa ya Sumbawanga km 5 kutoka Sumbawanga mjini, mbele ya timu ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Katika hali ya kuupendezesha mji wa Sumbawanga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameishauri wizara ya kilimo nchini kuona namna ya kuhamisha mradi wa ujenzi wa vihenge kutoka katikati ya mji wa Sumbawanga na kuhamishia katika eneo maalum lililotengwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwaajili ya ujenzi wa maghala na viwanda ili kuutanua mji na kujenga vihenge hivyo kwa nafasi.
Amesema kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)tayari wamekwishanunua eneo la ekari 24.6 lenye thamani ya shilingi 298,938,000 lililopo katika eneo maalum lililotengwa kwaajili ya viwanda vidogo, maghala na hotel lililopo Kijiji cha Kanondo, Kata ya Ntendo, Manispaa ya Sumbawanga ambapo mpaka sasa viwanja vilivyouzwa katika eneo hilo ni asilimia 35.
“Sisi tungependa kama mkoa wa Rukwa eneo hili liwekezwe, kwasababu tuna uchumi wa kati wa viwanda, lakini sasa naona bado tunapenda maeneo yet utu, sasa huku nani atakuja aendeleze? Kwakweli huu mradi uje kujengwa huku ntashauriana na wizara ya kilimo..Mh. Waziri..tuone namna ya kuleta huku, kwasababu hapo mnapotaka kujenga ni eneo dogo” Alisema.
Ameyasema hayo alipotembelea eneo hilo maaluma la uwekezaji wa maghala lililililonunuliwa na NFRA miaka miwili iliyopita huku likiwa limeachwa wazi bila ya matumizi yoyote.
Kwa upande wake Kaimu meneja wa NFRA Mkoa wa Rukwa James Marwa alisema kuwa mradi wa vihenge ulianza kabla ya kununuliwa kwa eneo hilo, hivyo ili kuhamisha mradi huo lazima eneo hilo jipya lipimwe upya.
Nae Afisa Mipango miji wa Manispaa ya Sumbawanga Thadeo Maganga amesema kuwa hatachoka kuendelea kuwahamasisha wadau mbalimbali kufika katika eneo hilo ili kuona umuhimu wake na kuweza kuwekeza kwa maslahi ya Manispaa, Mkoa nan chi kwa ujumla.
Ujenzi huo wa Maghala na Vihenge vya kisasa (Silos) utajengwa katika maeneo nane ya kanda saba za wakala ambapo ujenzi huo utaongeza uwezo wa kuhifadhi mahindi kutoka Tani 251,000 za sasa hadi Tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.
Mradi huo wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi umeanza kujengwa katika Manispaa ya Songea (Ruvuma), Dodoma, Mpanda (Katavi), Makambako (Njombe), Mbozi (Songwe), Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga Mjini (Shinyanga), na Babati (Manyara) ambapo Serikali ya Tanzania na Serikali ya Poland zilisaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na sh. bilioni 124, kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.
0 comments:
Post a Comment