Watu wawili wamefariki dunia papo hapo baada ya gari aina ya Totota Hiace walilokuwa wamepanda kuacha njia na kupinduka.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, George Kyando, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya alasiri. Aliwataja watu waliofariki katika ajali hiyo ni Augenia Masumbuko (53) mkazi wa Isale, na Nestory Kayumba mkazi wa Kalambo.
Kamanda huyo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T 795 CVA aina ya Toyota Hiace kushindwa kulimudu katika mteremko, hivyo kuacha njia na kupinduka.
Katika ajali hiyo watu wawili pia walijeruhiwa ambao ni Akoba Kung'ombe (40) mkazi wa Bangwe na mwingine ambaye hajafahamika ambaye ni mwanaume mwenye umri kati ya miaka 25-30.
Kamanda Kyando alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika kituo cha afya Namanyere, na majeruhi wamelazwa katika Zahanati ya Myula kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Kamanda Kyando, dereva wa gari hilo alikimbia baada ya ajali hiyo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili afikishwe mahakamani.
Aliwaasa madereva mkoani humo kwa makini wawapo barabarani na kufuata sheria za usalama barabarani, ili kuepuka vifo na majeruhi kutokana na ajali zinazoweza kuepukika.
0 comments:
Post a Comment