Idara ya elimu katika halmashauri ya wilaya ya SUMBAWANGA mkoani RUKWA imesajili
shule mbili za sekondari ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi zaidi ya
elfu moja mia tano waliokosa nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha
kwanza kwa ajili ya uhaba wa vyumba vya madarasa
Afisa elimu wa sekondari wa halmashauri ya wilaya
ya SUMBAWANGA, FANIKIO BITENDE amewaeleza
wakuu wa shule za sekondari kumi na moja wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya
ujenzi kuwa usajili huo utapunguza uhaba wa vyumba vya madarasa
vinavyohitajika kwa ajili ya wanafunzi elfu tatu mia sita thelethini na tisa
waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2018.
Amesema juhudi za uongozi wa serikali ya wilaya ya SUMBAWANGA kwa
kushirikiana na wadau wengine wa elimu zinalenga kuboresha miundo mbinu ya
kusomea katika shule zote za sekondari zilizopo ili kuwawezesha wanafunzi
wote elfu tatu mia sita na thelethini na tisa waliofaulu mtihani wa
darasa la saba mwaka 2018 kuendelea na masomo yao sekondari.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya SUMBAWANGA,
NYANGI MSEMAKWELI amewataka waratibu elimu kata kuhakikisha vifaa
hivyo vilivyotolewa kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa katika shule za
sekondari kumi na moja vinatumika ipasavyo.
Imeelezwa kuwa halmashauri ya wilaya ya SUMBAWANGA mkoani RUKWA imepanga
mikakati itakayowezesha wanafunzi wote walliofaulu mtihani wa darasa la saba
mwaka jana wanajiunga na masomo ya sekondari mwaka huu.
PETER KAPOLA SUMBAWANGA.
0 comments:
Post a Comment