Watu wanne, wakazi wa Kijiji cha Nzoka, Wilaya ya Momba mkoani Songwe wamefariki dunia kwa ugonjwa wa kimeta.
Jumla ya watu 81 wameugua ugonjwa huo baada ya kula nyama ya ng’ombe aliyekuwa na ugonjwa huo.
“Tumechukua hatua kwa kukusanya sampuli na kudhibitisha kuwapo wa ugonjwa wa kimeta,” Amesema Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile na kuongeza;
“Mpaka (leo) jana, hakuna ongezeko la wagonjwa wapya na waliopo wameshapatiwa matibabu.
“Januari 3 tulipata taarifa ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa huu katika Kijiji cha Nzoka na mpaka sasa taarifa zilizopo ni kwamba wagonjwa 81 waligunduliwa na kati yao wanne wamefariki.”
Dk Ndugulile alisema taarifa walizopata kutoka Songwe ni kwamba wananchi waliuziwa nyama kwa bei ya Sh500 kwa kilo na baada ya kula waliugua ugonjwa huo.
Kwa kawaida kilo moja ya nyama katika eneo hilo ni Sh4,000 lakini nyama iliyosababisha maradhi hayo iliuzwa kwa mapande ambako kila moja liliuzwa kwa Sh500 kutokana na mifugo mingi kufa.
Dk Ndugulile alitoa tahadhari kwa wananchi, “Waache mara moja kununua nyama ambayo hawajui chanzo chake. Lazima ukae uhoji, wananchi waende kununua nyama katika bucha zilizodhibitishwa na Serikali.”
Alisema kwa sasa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo inaangalia namna ya kutoa chanjo kwa mifugo katika eneo hilo ili kuondoa kabisa vimelea vya ugonjwa huo kwa wanyama.
“Bado tunaendelea kutoa elimu kwa waathirika wa ugonjwa huu. Wawakilishi wetu wamekuwa wakitoa elimu hii maeneo ya mikusanyiko ya watu na wale wanaopatiwa matibabu hospitalini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment