RUBANI wa ndege ndogo, mkazi wa Dar es Salaam, David Mbale (25),
amefariki dunia baada ya ndege aliyokuwa akiendesha kuanguka kwenye
vilima vya Monduli mkoani Arusha.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema tukio hilo
lilitokea juzi katika Kijiji cha Engalaoni kilichopo mpakani mwa wilaya
za Monduli na Arumeru.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, Mbale alikuwa akiendesha ndege ndogo yenye
namba za usajili 5HSAL 206 inayomilikiwa na Kampuni ya Safari Air Link.
“Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria watano, iliondoka katika uwanja
mdogo wa ndege wa Arusha, majira ya saa 1:30 asubuhi ya siku hiyo ya
tukio ikielekea katika eneo la Kogatende, Serengeti kuwachukua watalii.
“Kwenye ndege hiyo, alikuwamo rubani peke yake na alikuwa anasubiriwa na watalii huko Serengeti.
“Taarifa za kuanguka kwa ndege hiyo zilianza kuenea juzi saa nne
asubuhi, zikisema kuna ndege imeanguka katika vilima vya Monduli ambavyo
ni maarufu kama Monduli Hills.
“Baada ya taarifa hizo kutolewa saa 6:30, tuliwajulisha kikosi cha
zimamoto na wenzetu wa uwanja wa ndege wa Arusha na walipofika kwenye
kilima hicho, walikuta rubani ameshafariki dunia na mwili wake
ulichukuliwa kwa uchunguzi zaidi,” alisema Kamanda Mkumbo.
Wakati huo huo, Kamanda Mkumbo alisema uchunguzi wa tukio hilo umeanza
jana na kwamba watashirikisha wataalamu waliobobea katika masuala ya
ndege.
0 comments:
Post a Comment