WATU 11 wanashikiliwa na Polisi mkoani
Dodoma akiwemo mganga wa jadi, Ashura Matha (33), wakituhumiwa kuhusika
na kifo cha Mariam Saidi (17) aliyeuawa kikatili kwa kukatwa shingo,
kutenganishwa kiwiliwili na kuchomwa moto kichwa na sehemu za mwili
wake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP), Lazaro Mambosasa alisema mwili wa Mariam ulikutwa nyumbani kwa
mganga huyo wa jadi katika kitongoji cha Chang’ombe Kijiji cha
Chamwino-Ikulu wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Kamanda Mambosasa alisema mauaji ya Mariam ambaye ni mwenyeji wa Kigoma,
yalifanyika juzi saa nne 4.00 usiku katika kitongoji hicho, ambako
wauaji walimkata shingo, wakatenganisha na kiwiliwili, wakachoma moto
kichwa na kubakia fuvu lisiloweza kutambuliwa sura yake. Pia baadhi ya
sehemu za mwili ukiwamo mkono wa kushoto, shingo, kifua na sehemu za
siri ziliunguzwa vibaya.
Alisema mazingira ya tukio hilo mahali lilipotokea, yanaonesha kwamba
mganga huyo wa jadi asiye na kibali cha kuendesha shughuli za tiba
asili, pia analaza wagonjwa nyumbani kwake, anawafanyia matambiko,
anapiga ramli chonganishi na anafanya tohara kwa watoto. “Kutokana na
tukio hilo, Jeshi la Polisi pia linawashikilia watu wanane ambao
walikuwa wamelazwa katika nyumba hiyo siku ya tukio wakiwamo wanawake
sita na wanaume wawili,” alisema.
Kamanda Mambosasa na kuongeza kuwa waliwakamata watu wengine wawili
ambao ni Msaidizi wa mganga wa jadi, Victor Chibelenje (24) ambaye ni
mkazi wa kitongoji cha Mwongozo, Kijiji cha Chamwino na mume wa mganga
huyo na Noel Mazengo ambaye ni mkazi wa Chang’ombe, katika kijiji cha
Chamwino- Ikulu.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo la kusikitisha
na pia kuchunguza namna ambavyo Mariam alifika kijiji hicho kutoka
mkoani Kigoma. Kamanda wa Polisi alisema jeshi lake linalaani tukio hilo
baya na la kinyama na hakikubaliki mahali popote, ni fedheha kubwa kwa
wana-Chamwino kuendelea kukumbatia imani za kushirikina katika karne
hii, hasa wakati serikali imesogeza huduma muhimu za afya karibu na
maeneo ya jamii.
Alitoa mwito kwa waganga wa jadi wote wanaoendesha ramli chonganishi
katika maeneo mbalimbali ya jamii, wafichuliwe ili wakamatwe na
kuchukuliwa hatua kabla hawajaufikisha mkoa katika hatua mbaya na ya
fedheha zaidi. Wakati huohuo, mkazi wa Kijiji cha Ntyuka Kata ya Ntyuka
katika Manispaa ya Dodoma, Masumbuko Nyerere (24), amekufa kwa kufunikwa
na kifusi cha mchanga. Kamanda Mambosasa alisema ajali hiyo ilitokea
juzi saa 1.00 asubuhi kijijini hapo katika eneo la machimbo hayo baada
ya kufukiwa na kifusi cha mchanga wakati anachimba.
0 comments:
Post a Comment