WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka maofisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato
Tanzania (TRA) wakusanye kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na
wasitoze kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.
“TRA
ijipange kukusanya kodi za majengo kuanzia Julai mosi 2017. Katika
kutekeleza jukumu hilo, zingatieni sheria. Tusisikie mnawadai kodi ya
majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 kwa majengo wanayotumia kama
makazi yao,” alisema Majaliwa.
Alitoa
agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa Wilaya ya
Chato waliohudhuria uzinduzi wa jengo la TRA wilayani humo mkoani
Geita. Waziri Mkuu amewataka moafisa hao wakusanye kodi ya majengo
kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini kwani kodi hiyo haiwahusu.
“Msiende
vijijini. Nyumba za nyasi au za tembe hazihusiki. Tembeleeni nyumba za
mijini. Piteni kwenye mitaa, muainishe aina zote za nyumba zinazostahili
kulipiwa kodi. Mkishafanya sensa, wekeni utaratibu wa kuwawezesha
wananchi kulipia kodi hizo,” alisema huku akishangiliwa.
Pia aliwataka wananchi wanaonunua bidhaa wadai risiti lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye kiwango halisi walicholipia.
“Ukipewa
risiti uiangalie kama ina kiwango halisi cha fedha uliyotoa.Kuna watu
wachache wasio waaminifu wanaamua kukupa risiti, lakini imeandikwa bei
ndogo kuliko ile uliyolipia, ukitoa laki moja anakupa risiti ya shilingi
elfu kumi,” alieleza.
Mapema,
akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja, Kamishna Mkuu
wa TRA, Charles Kicheere alisema ujenzi huo ulianza Julai 12, mwaka jana
na ulikamilika Juni 12, mwaka huu.
“Ujenzi
wa jengo hili umegharimu Sh bilioni 1.4 na ulichochewa na ongezeko
kubwa la idadi ya walipakodi wa Chato kutoka watu 150 mwaka 2010/11 hadi
kufikia watu 600 mwaka 2016/17,” alieleza.
Pia
alisema wamejenga ofisi hizo ili kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa
wilaya hiyo ambao walilazimika kwenda Geita mjini kupata huduma za TRA
ambako ni umbali wa zaidi kilometa 120.
Alisema
hivi karibuni watakamilisha ukarabati wa ofisi za mikoa ya Mara, Iringa
ikiwemo kujenga ofisi kwenye mikoa mipya ya Simiyu, Katavi, Njombe na
Manyara. “Pia tutajenga ofisi kwenye mkoa mpya wa kikodi wa Kahama,”
alieleza.
Alizitaja
wilaya ambazo ziko mbioni kupatiwa ofisi zake kuwa ni Kondoa, Longido,
Bunda na Arumeru. Alisema katika mwaka ujao wa fedha, TRA imelenga
kukusanya Sh trilioni 17.106 na watahakikisha wanafikia lengo hilo.
0 comments:
Post a Comment