Taarifa kutoka magharibi mwa Kenya
zinasema kuwa mtuhumiwa wa wizi wa gari alijisalimisha kwa polisi baada
ya kuvamiwa na nyuki akiliendesha gari hilo.
Mwandishi wa BBC, Wanyama wa Chebusiri
kutoka Nairobi, anasema ripoti hiyo iliyoripotiwa mara ya kwanza kwenye
gazeti la The Star la nchini Kenya, imewaacha wengi vinywa wazi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwenye gari
aliamini kwamba mshukiwa alimuwekea dawa ya kulevya kwenye kinywaji
katika hoteli moja na kumfanya apoteze fahamu.
Saa kadha baada ya kurejelewa na fahamu, alipata gari lake halipo.
Mwenye gari alitafuta msaada wa mganga
wa kienyeji ambaye alimhakikishia kwamba mtuhumiwa atavamiwa na nyuki
kabla ya kuondoka katika mji wa Bungoma ulioko magharibi mwa Kenya.
Punde si punde, nyuki walimvamia
mshukiwa akiwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara
moja maarufu mjini Bungoma.
Katika harakati za kutaka kujinusuru
kutoka kwa makali ya nyuki, mshukiwa alichana mbuga akielekea kituo cha
polisi cha Bungoma, huku akipiga kelele za niokoe lakini wapi, nyuki
walikuwa naye 'hapa kwa hapa'.
Mwanamme huyo alijaribu kutoka katika
kituo cha polisi lakini nyuki walimwandama unyonunyo kabla ya polisi
kumuokoa kwa kumfungia ndani ya seli kwa mahojiano.
Mkuu wa polisi katika eneo la Bungoma
David Kirui ameiambia BBC kwamba nyuki walikuwa wamezingira kituo hicho
cha usalama huku mshukiwa akiwa anahojiwa kwa madai ya wizi wa gari.
Kisa hiki cha nadra kiliwastajabisha na kuwashangaza wakaazi wengi
wakiachwa vinywa wazi, huku wengi wa kijiuliza, je, ushirikina ungalipo?
0 comments:
Post a Comment