Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakanusha taarifa
zilizoandikwa na gazeti la HABARILEO toleo la tarehe 19 Juni, 2017,
kwamba wasichana 2,892 waliokuwa wanafunzi wa shule za msingi wilaya ya
Nkasi, mkoani Rukwa walikatishwa masomo yao kutokana na tatizo la mimba
na ndoa za utotoni kwa kipindi cha mwaka 2016.
Taarifa sahihi aliyoitoa Afisa
Maendeleo ya Jamii wa wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Bi. Mary Siyame,
wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu,
ni “kwamba kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2016 jumla ya watoto 9,723
waliandikishwa shule, wavulana wakiwa 4,806 na wasichana 4,917 katika
wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa.
Kwa kipindi hicho (2010-2016) wavulana
2,991 waliacha masomo na wasichana 2971, kutokana na sababu mbalimbali
ikiwa ni pamoja na utoro, kuhama, kupata mimba na ndoa za utotoni.
Aidha, kwa kipindi cha mwezi
Januari hadi Juni 2017 wasichana 8 wanafunzi wa shule ya msingi na
wasichana 22 kwa upande wa shule za sekondari walikatisha masomo yao kwa
sababu ya kupata mimba na ndoa za utotoni.
Kufuatia taarifa hii, Wizara
inasahihisha taarifa ya gazeti la HABARILEO ili kuondoa mkanganyiko
unaoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya takwimu zisizokuwa sahihi
kuhusu idadi ya wasichana waliokatisha masomo kutokana na mimba na ndoa
za utotoni katika wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa kwa kipindi cha mwaka
2016.
Ifahamike kuwa miongoni mwa
shabaha kuu za Serikali nchini ni kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoacha
shule kutokana na kupata mimba kwa asilimia 50 ifikapo Juni 2022,
kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 27 hadi asilimia 5, na
kuongeza msaada wa kielimu kwa wasichana wanaotoka katika familia
maskini kutoka asilimia 23.4 hadi asilimia 53.4.
Aidha, Wizara kupitia kitini cha
Malezi kwa Familia itaendelea jitihada za kutoa elimu ya malezi kwa
wazazi, sambamba na kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Dhamira ya Wizara ni kuona kuwa
wadau katika ngazi zote tunashiriki kuzuia mimba na ndoa za utotoni ili
kuimarisha upatikanaji wa fursa ya elimu, ulinzi na malezi bora kwa
watoto wetu wa kike wakiwemo watoto wa wilaya ya Nkasi na maeneo nchini.
Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
23/6/2017
0 comments:
Post a Comment