MADIWANI SONGWE WAMTIMUA MKURUGENZI KWA UTENDAJI MBOVU

 
Mkurugenzi Wa Wilaya ya Songwe aliyeondolewa na baraza LA madiwani akisoma ajenda za kikao
 
Madiwani wakinyosha mikono juu kuashiria kuunga mkono hoja ya kutokua na imani na mkurugenzi Wa Halmashauri.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mkoani Songwe limepitisha azimio la kutokuwa na imani na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Elias Nawera kwa kile kilichodaiwa kushindwa kutimiza wajibu wake.

Baraza hilo lilipitisha azimio hilo katika kikao cha dharula kilichofanyika juzi katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri, Abraham Kagaluka aliwasilisha taarifa mbele ya baraza la madiwani.

Akiwasilisha hoja yake Mwenyekiti huyo alisema  Mkurugenzi huyo tangu Halmashauri iundwe Septemba 15, 2016 ameshindwa kutekeleza maazimio mbali mbali anayoagizwa na Baraza la madiwani pamoja na kukosa ushirikiano na Wakuu wa Idara.

Kagaluka alisema kikao cha Kamati ya Fedha na mipango kilichoketi Oktoba 13, 2016 kilibaini mapungufu ya kiutendaji ya Mkurugenzi na uwepo wa migogoro baina ya Wakuu wa Idara na watumishi hali iliyopelekea kuudhofisha halmashauri.

Alisema baada ya kikao hicho Kamati ilimuonya Mkurugenzi kuacha kusababisha migogoro ambapo aliomba radhi na kukiri lakini hali hiyo ilijitokeza tena katika kikao cha Novemba 15,2016 na ndipo Kamati iliamua kumhoji mtumishi mmoja mmoja.

Alisema baada ya kuwahoji watumishi wote akiwemo Mkurugenzi ilibainika kuwa asilimia 90 ya migogoro inasababishwa na Mkurugenzi huku asilimia 10 ikisababishwa na Afisa Utumishi wa Halmashauri ambapo alisema Kamati iliwapa onyo kali na wao kukiri kwa maandishi.

Mwenyekiti huyo alisemna Kikao cha Kamati ya Fedha na mipango kilichoketi Disemba 12,2016 kilipokea taarifa ya kubomoka kwa daraja la Kikamba na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya baadhi ya vijiji pa moja na kuharibika kwa barabara ya Galula.

Alisema kikao kilikubaliana na kumuagiza Mkurugenzi kuandika barua kwenda ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Songwe kuomba kubadilisha vifungu ili kupata fedha za kurudisha miundombinu iliyoharibika kwa fedha za dharula.

Alisema tangu wakati huo hadi sasa hakuna barua iliyoandikwa na miundombinu haijatengemaa hali iliyopelekea ajali kutokea na kusababisha majeruhi sita katika barabara ya Galula ambapo pia Wakazi wa Gua kuishi kisiwani kutokana na daraja la Kikumba kutotengenezwa.

Alisema Mkurugenzi alifanya kikao cha Watumishi (CMT) kwa lengo la kuchagua waliokuwa wakikaimu idara ili baraza la madiwani liwaombee kuthibitishwa kuwa wakuu wa idara jambo ambalo lilifanyika na majina kupelekwa kwa Madiwani na kuyapitisha.

Alisema baada ya kupitisha majina hayo, Mkurugenzi aliandika barua kwa RAS Novemba 22, 2016 akiomba kubadilishiwa majina hayo kwa kile alichodai Madiwanbi walimchagulia na kumlazimisha kuchagua watumishi hao.

Mwenyekiti huyo alisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa kanuni wa kubadili maazimio ya Baraza na kuandika anachojua yeye pia kulichanganisha Baraza na mamlaka zingine jambo linalopekea kuzolotesha maendeleo ya Wilaya.

Aliongeza kuwa Kamati ya Fedha aliagiza kujengwa kwa karakana ya ufundi magari katika maeneo ya Halmashauri ili kupunguza gharama zinazopelekea magari kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matengenezo lakini jambo hilo halijatekelezwa hadi sasa.

Alisema pia Mkurugenzi aliomba kibali cha kuajiri wahudumu 3 na Madereva 3 kutoka kwenye kamati jambo ambalo alikubaliwa lakini hakufuata utaratibu wa ajira ambapo alitafuta madereva kinyemela kisha kuwakabidhi magari mapya ambayo yote yameangushwa na hajatoa taarifa yoyote.

Wakichangia hoja hiyo baadhi ya Madiwani wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Songwe(CCM), Philipo Mulugo walisema Mkurugenzi ameshindwa kuwaunganisha watumishi na amekuwa akikaimisha ofisi mara kwa mara.

Walisema Mkurugenzi hana ushirikiano na ofisi ya Mbunge, Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na Mkuu wa Wilaya jambo linalohatarisha ukuaji na ustawi wa Halmashauri hiyo.

Mbunge Mulugo alisema Baraza haligusi Ukurugenzi wake wala mamlaka iliyomteua bali hawako tayari kufanya nae kazi hivyo ahamishwe na kupangiwa sehemu nyingine.

“Ieleweke wazi kuwa hatugusi Ukurugenzi wake bali hatuko tayari kufanya nae kazi wakupeleke sehemu nyingine sisi watuletee Mkurugenzi ambaye anaweza kuendana na kasi yetu” alisisitiza Mbunge.

Walisema Mkurugenzi huyo hakushiriki kikao cha kupitisha bajeti hivyo hadi sasa haijui bajeti ya Halmashauri, pia walisema aligoma kusafirisha madawati yaliyotolewa na Bunge sambamba na kuwakatisha tama wawekezaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alipopewa nafasi ya kujitetea alipinga tuhuma hizo na kwamba anaonewa kwani yeye hafanyi kazi za siasa bali anatekeleza majhukumu yake kwa mujibu wa taratibu.
Akifunga hoja hiyo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya SongweIsaya Ndolomi alisema kati ya Madiwani 26 ni Madiwani 23 waliohudhuria kikao hicho na wote kwa pamoja kuunga mkono hoja kwa kuandika majina yao na kusaini.

Alisema kwa maana hiyo Mkurugenzi hataruhusiwa kuingia ofisini hapo hapo mamlaka zinazohusika zitakapotoa maelekezo mengine juu ya nini kifanyike ambapo Kamati ya Fedha itafanya utaratibu wa kumteua mtumishi wa kukaimu.
posted by peter kapola 0764033168
  
Share on Google Plus

About KAPOLA NEWZ TV..✍️

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment