Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametoa
ufafanuzi juu ya kauli iliyonukuliwa ikionyesha kuwa alipinga vita dhidi
ya dawa za kulevya iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda. Amedai kuwa hakupinga vita hiyo bali alitaka busara itumike
kwa washukiwa.
Waziri Nape alitoa ufafanuzi huo katika kipindi cha dakika 45 cha ITV,
alipoulizwa swali na mtangazaji wa kipindi hicho kutaka kujua kuhusu
kauli yake iliyoonesha kupinga utaratibu uliotumika wa kuwakamata au
kuwapata watuhumiwa wa dawa za kulevya.
“Niseme kwanza ilitokea nilikuwa na mkutano na waandishi wa habari,
ukienda leo ukanitaja Nape ukaniambia baada ya siku mbili njoo kituoni,
hata kama nilikuwa na madawa ya kulevya nyumbani kwangu hivi
unayakutaje? Kwasababu kwa vyovyote vile nitayachukua, ntayaficha,
ntakuja kituoni ntaripoti utanibana ntakwambia twende nyumbani kwangu
ukakague mnaenda mnakagua mnakuta hamna, si basi! Kwahiyo nikawa na
wasiwasi kwamba inawezekana kabisa nia ilikuwa njema lakini nilidhani
pangeweza kutengenezwa utaratibu bora zaidi ya namna ya kuwapata,
kwasababu hapa kuna watumiaji, kuna wauzaji na wale ambao wanaleta sasa
madawa ya kulevya,” alisema Nape.
Aliendelea, “Ukishughulika na mtumiaji huyu ukadhani ndiye mhalifu
wako unakosea, kwasababu huyu ni muathirika na muathirika anahitaji dawa
anahitaji huduma ameshaathirika, hapa wahalifu wetu nikuanzia huyu
anayemletea halafu kuna huyu anayempa yule aliyemletea, sasa ili uwapate
hawa wawili lazima umtumie huyu vizuri ili akupeleke kwa hawa wawili.
Lakini ukimkamata huyu ukamtia ndani sasa hawa wawili watakimbia.”
“Kwahiyo mimi nikaona kwamba tunaivuruga vita yenyewe, anayeingiza
madawa ya kulevya na anayesambaza kwa maana ya kuyauza, hawa ndiyo
tatizo letu. Na ndio maana nikasema hebu tutumieni busara, watu
wakadhani nimepinga. Tena mimi nilisema mara nyingi sana tumieni busara
namna ya kuiendesha vita hii.
Madhara ya kutotumia busara katika vita
hii ni makubwa sana, kwasababu ukimweka huyu mtu mmoja ndani hawa
wengine wataendelea kuwaathiri wengine na ndiyo maana nasema hii vita
tutumieni busara. Hii vita ni ya kupigana kimya kimya kwasababu
wanaofanya biashara hii hawaifanyi hadharani wanafanya kwa kificho.
Shughulika nao kwa kificho, hii vita hakuna mahali ambapo wameshawahi
pigana hadharani, tukitajana hadharani hata wenye chuki watatajana humo
humo,” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment