MUUGUZI anayefanya kazi Kituo cha
Afya Kata ya Igurubi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Damian Mgaya (26)
anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma ya kumbaka binti wa miaka 18 mkazi wa
Kijiji cha Mwagala.
Mtendaji wa Kata ya Igurubi, Ntemi James
alisema uhalifu huo umefanyika Julai 14, mwaka huu saa 8 hadi alfajiri
wakati binti huyo akimuuguza mama yake, ambaye amelazwa katika kituo
hicho cha afya baada ya kushambuliwa kwa kipigo na mume wake.
James alidai mtuhumiwa alimpokea mama
wa binti huyo akiwa hoi na ndipo alimpatia matibabu kisha kumlaza katika
kituo hicho cha afya huku akimchoma sindano ya usingizi ambayo
ilisababisha mama huyo kupitiwa na usingizi.
Mtendaji huyo alidai kuwa muuguzi Damian
alipoona mama wa binti huyo amelala, alimwambia waende wote chumba
kingine ili akachukue dawa ya mama yake; lakini hata hivyo hakumpa dawa
na badala yake alimwambia amchome sindano ili asipate maradhi kwa kuwa
mazingira ya hospitali sio mazuri.
Baada ya kuambiwa hivyo, binti huyo
alikubali kuchomwa sindano mbili na alipochomwa sindano ya kwanza
aliishiwa nguvu na alipochomwa sindano ya pili alianguka na kupitiwa na
usingizi hadi asubuhi.
Alisema baada ya kuona amelala
pasipokuwa na fahamu, muuguzi huyo alianza kumbaka hadi alfajiri
alipoamshwa na mama yake huku yeye akiwa hajitambui kutokana na maumivu
aliyokuwa akiyasikia sehemu zake za siri na mwili wote.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga,
Bonaventura Kalumbete alithibitisha kubakwa kwa binti huyo na muuguzi
huyo na kueleza kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, alituma timu ya
wataalamu ambayo ilibaini binti huyo kubakwa na amelazwa kwenye kituo
hicho na hali yake ni mbaya kwani hawezi kutembea.
Aidha, Dk Kalumbete alisema uchunguzi wa
awali unaonesha binti huyo alichomwa sindano wakati alikuwa hata haumwi
na hizo dawa nazo zimechangia kumsababishia kushindwa kutembea huku
akiahidi kuwa baada ya uchunguzi, muuguzi huyo atachukuliwa hatua kali
za kisheria.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, John Mwaipopo
alikiri kukamatwa kwa muuguzi baada ya kupokea taarifa ya kubakwa kwa
binti huyo, alimwagiza Mkuu wa Polisi Igunga kumkamata muuguzi huyo
Damian Mgaya ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
0 comments:
Post a Comment