VIONGOZI WA SOKA RUKWA WATIWA HATIANI, WATATU KILA MMOJA WAFUNGIWA MWAKA MMOJA

 

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewatia hatiani viongozi watatu akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA), James Thomas Makwinya.
Viongozi wa RUREFA waliotiwa hatiani ni pamoja na Blassy Kiondo na Kaimu Katibu Mkuu, Ayoub Nyauringo ambao Kamati ya Nidhamu chini ya Mwenyekiti Abbas Tarimba iliyosikiliza shauri hilo zaidi ya mara tatu kabla ya kufikia uamuzi.


Blassy Kiondo
Baada ya Blassy Kiondo kutiwa hatiani, Kamati imechukua uamuzi wa kumfungia kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje kwa mwaka mmoja kwa mujibu wa kanuni za nidhamu za TFF, Kanuni ya 64 (4) na inamuamuru kulipa faini ya Sh. 1,000,0000 (Milioni moja) kwa mujibu wa Kanuni ya ya 64 (1) (a) ya Kanuni za nidhamu za TFF. Mlalamikiwa ana haki ya kukata rufaa kama kanuni zinavyoelekeza.

Awali, Kiondo alilalamikiwa na TFF kuwa alishindwa kuheshimu uamuzi halali wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF kinyume cha kanuni ya 64 ya kanuni za Nidhamu za mwaka 2012.


Kwamba akiwa Mwenyekiti wa RUREFA, anadaiwa kuwa kati ya Desemba 2016 na Januari 2017, alipuuza maelekezo ya kusimamisha uchaguzi wa RUREFA hadi hapo rufaa zilizokuwa zimekatwa kuamuliwa. Kadhalika, Kiondo alishiriki katika uchaguzi huo.


Ayoub Nyauringo
Kamati kwa kauli moja, imemtia hatiani Ayoub Nyauringo amefungiwa kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa muda wa mwaka mmoja chini ya Kanuni ya 64(4)  za nidhamu za TFF. Hiyo ni adhabu kama alivyoshitakiwa ili iwe fundisho kwa viongozi wengine katika kutii maagizo wanayopewa na ngazi za juu za uongozi. 


Awali, Nyauringo alilalamikiwa na TFF kuwa alishindwa kuheshimu uamuzi halali wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF kinyume cha kanuni ya 64  ya kanuni za Nidhamu za mwaka 2012.


Kwamba akiwa Kaimu Katibu wa RUREFA, anadaiwa kuwa kati ya Desemba 2016 na Januari 2017, alipuuza maelekezo ya kusimamisha uchaguzi wa RUREFA hadi hapo rufaa zilizokuwa zimekatwa kuamuliwa.


Katika utetezi wake, Nyauringo mbele ya Kamati ya Nidhamu ya TFF alikiri kupokea barua ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi kama ilivyoagizwa, lakini ushauri wake haukufanyiwa kazi wala kusikilizwa bali aliambiwa kwamba Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA inafanyia kazi na uchaguzi upo pale pale.


Kamati baada ya kupitia ushahidi wote imejiridhisha bila shaka yoyote kuwa mlalamikiwa alitenda kosa analoshitakiwa nalo na kushindwa kuheshimu uamuzi wa TFF; sababu zikiwa ni nyingi ikiwamo kukiri kuwa mchakato wa uchaguzi ulisitishwa sambamba na kukosa Mwakilishi kutoka TFF. Mlalamikiwa ana haki ya kukata rufaa kama kanuni zinavyoelekeza.


James Makwinya
Kuhusu James Makwinya, Kamati inamtia hatiani mlalamikiwa kwa makosa mawili kama alivyoshitakiwa na TFF. Kwamba Mlalamikiwa alishindwa kuheshimu uamuzi halali  wa Kamati ya Uchaguzi  ya TFF na vilevile imethibitishwa kuwa alitoa lugha isiyo ya kiungwana na kiuanamichezo kama ushahidi unavyooneshwa hapo juu.

Katika shitaka la kwanza mlalamikiwa anafungiwa kutojihusisha kwa namna yoyote ile na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kipindi cha mwaka mmoja kwa mujibu wa Kanuni ya 64 (4) ya kanuni za nidhamu za TFF pamoja na kulipa faini ya Sh. Milioni moja kwa mujibu wa kanuni ya 64 (1) (a)ya kanuni za nidhamu.


Hii ni kwa sababu imethibitika kuwa mlalamikiwa alipokea barua ya Desemba 19, 2016 iliyomtaka kusitisha mchakato wa uchaguzi wa RUREFA. Alikaidi maagizo hayo na kuendeleana uchaguzi bila uhalali wowote na bila kuwepo mwakilishi yeyote kutoka TFF. Mlalamikaji ana haki ya kukata rufaa kama kanuni zinavyoelekeza.

Share on Google Plus

About KAPOLA NEWZ TV..✍️

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment