Mwenyekiti
wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja, amelaani
kitendo cha kutishiwa kwa silaha ya moto aliyekuwa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Vijana, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Amesema
kwamba, kitendo kilichofanyika dhidi ya Nape ni ukiukwaji wa haki za
kibinadamu na utawala bora ambacho hakiwezi kuvumiliwa.
Mgeja,
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, kabla hajahamia
Chadema mwaka juzi, alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari mkoani Kigoma.
Pamoja na hayo, alimuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, asimame hadharani kuwaomba radhi Watanzania kwa niaba ya Serikali.
“Mbali
ya kuwaomba radhi Watanzania, waziri mkuu achukue hatua mara moja ya
kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo kuheshimu
misingi ya demokrasia kwa kuzingatia katiba ya nchi, sheria, kanuni na
taratibu,” alisema Mgeja.
Akifafanua
zaidi, mwanasiasa huyo alisema tukio la Nape kutishiwa silaha ni moja
ya matukio ya ukandamizaji wa haki za binadamu yanayoendelea kutokea
nchini na kwamba yanatakiwa kukemewa kabla hayajaleta madhara zaidi kwa
wananchi.
“Kwa
kweli mimi binafsi pamoja na taasisi yangu ya Tanzania Mzalendo
Foundation, tunalaani vikali kitendo kilichotendwa hadharani na mmoja wa
walinzi wa raia.
“Yaani
kitendo cha kumtisha raia kwa silaha ya moto kwa lengo tu la kumzuia
asizungumze na wanahabari hakikubaliki, tukio hili limetushtua na
kutusikitisha Watanzania.
“Matukio
haya ni ishara ya wazi ya ukandamizaji wa demokrasia na ni matumizi
mabaya ya madaraka ambayo yameanza kushika kasi miongoni mwa viongozi wa
Serikali.
“Wananchi
wengi hivi sasa hawatendewi haki, angalieni yanayotokea kwa wafugaji,
ikiwamo tukio la hivi karibuni ambalo vijana wawili wa kifugaji kule
Bagamoyo walipigwa risasi na kufariki.
“Wananchi
wanyonge hivi sasa wanajiuliza iwapo mtu aliyekuwa waziri wa Serikali
na kada maarufu ndani ya chama tawala na aliyekipigania kiweze kupata
ushindi japokuwa kwa goli la mkono, leo anafanyiwa vitendo vya aina
hiyo.
“Kwa
kuwa sikufurahishwa na tukio hilo, namshauri Waziri Mkuu Majaliwa,
asimame hadharani kwa niaba ya Serikali ya CCM, awaombe radhi
Watanzania.
“Tena
awahakikishie matukio ya aina hiyo hayajirudii tena kwa sababu yeye na
viongozi wengine, waliapa kuilinda Katiba na siyo kuivunja,” alisema Mgeja.
0 comments:
Post a Comment