NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
kuanzisha kituo cha zimamoto Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Masauni alisema Aprili Mosi
mwaka huu Jeshi hilo litakuwa na ofisi wilayani humo ili askari wa Jeshi
hilo waanze kutoa huduma sehemu mbalimbali ya Wilaya hiyo ambayo ni
muhimu kituo hicho kuwepo kutokana na uwepo na machimbo ya madini ya
dhahabu pamoja na mji kuendelea kukua kwa kasi.
“Tumekubaliana vizuri baada ya
Kamanda wa Zimamoto mkoa kuwa ifikapo tarehe moja askari wa zimamoto
watakuwepo hapa Ruangwa rasmi kwa ajili ya kuanza kazi, na watapewa
ofisi na halmashauri ya Wilaya, hivyo utaratibu wa kupata vifaa vya
awali uanze mara moja kama tulivyokubaliana,” alisema Masauni.
Kwa upande wake Kamanda wa
Jeshi hilo Mkoa wa Lindi, Christina Sunga alimuhakikishia Naibu Waziri
pamoja na Watendaji wa Wilaya hiyo, agizo hilo atalifanyia kazi haraka
iwezekanavyo na mpaka ifikapo Aprili mosi mwaka huu tayari askari wawili
watakuwa wameripoti mjini Ruangwa.
“Uwepo wa askari hawa
kutarahisisha kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa umma jinsi ya kuzima
moto pamoja na kupambana na uzimaji moto, licha ya kuwa tunakuwa na
vifaa vya awali vya uzimaji moto mpaka hapo tutakapopata gari kwa ajili
ya shughuli mbalimbali za uzimaji moto na utoaji elimu zaidi,” alisema
Sunga na kuongeza;
“Tunashukuru Halmashauri ya
Wilaya ya Ruangwa kwa kutupa ofisi kwa ajili ya askari wa zimamoto
lakini pia kutuwezesha kupata vifaa hivyo vya awali vya uzimaji wa
moto.”
Aidha, Masauni alimuagiza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, (RPC) Renatha Mzinga kuandaa mchoro
pamoja na gharama ya ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi cha Wilaya ya
Ruangwa ili ujenzi huo uanze.
“Nimekagua eneo la ujenzi wa
kituo kipya cha polisi, eneo zuri na linafaa kwa ujenzi wa kituo kikubwa
cha polisi, maandalizi tayari yameanza na hivi karibuni RPC
atakamilisha mchoro pamoja na gharama ya ujenzi wa kituo hicho hapa
Ruangwa,” alisema Masauni.
Pia Masauni amesema Wizara
yake itahakikisha inawajengea ofisi Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (Nida) pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani humo
ambapo kwasasa ofisi hizo zipo katika jengo la Halmashauri ya Wilaya
hiyo.
Naibu WaziriMasauni amemaliza
ziara yake ya siku mbili kwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo
pamoja na kuzungumza na askari na maafisa wa vyombo walio chini ya
wizara yake mkoani Lindi na tayari amesafiri mkoani Mtwara kuendelea na
ziara yake.
0 comments:
Post a Comment