MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amemuagiza Kaimu Mganga Mkuu wa
mkoa huo, Dk Emmanuel Mtika, ahakikishe mtoto Peter Kazumba (13)
anayesumbuliwa na ugonjwa sugu wa ngozi, anapelekwa haraka katika
Hospitali ya Mkoa wa Rukwa iliyopo Sumbawanga mjini kwa matibabu.
Mtoto Peter ambaye hasomi na hajawahi kuingia darasani anaishi na
wazazi wake katika kitongoji cha Nkata kilichopo katika Kata ya Kate
wilayani Nkasi, anasumbuliwa na ugonjwa sugu wa ngozi kwa zaidi ya miaka
mitano bila kupona.
Ugonjwa huo umemfanya aharibike na kutoa harufu
kali, huku akiwa na jeraha kubwa la moto katika goti lake la mguu wa
kushoto na anaonekana mzee kuliko umri wake.
Aidha, Zelothe aliwataka wakazi wa kitongoji hicho, kuacha
kumnyanyapaa mtoto huyo pamoja na familia yake ya watu wote wanane,
akiwemo baba na mama mzazi na watoto wengine watano akiwemo mtoto mwenye
umri wa mwaka mmoja wameambukizwa ugonjwa huo.
Zelothe alitoa maagizo
hayo baada ya kufika katika kitongoji hicho na kujionea mwenyewe jinsi
mtoto huyo anavyoteseka kwa kuugua ugonjwa huo, ambao madaktari wanadai
hauambukizi.
Mkuu huyo wa Mkoa alilazimika leo kufunga safari hadi katika
kitongoji cha Nkata, ikiwa ni siku moja baada ya gazeti hili kuripoti
habari ya mtoto huyo na familia yake, ambayo imetengwa na wakazi wa
kijiji hicho kwa hofu ya kuambukizwa.
Aliongozana na Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mtika na Mratibu
wa Ukoma na Kifua Kikuu mkoa wa Rukwa, Dk Dismas Buhiri.
“Acheni
kuinyanyapaa familia hii wala nisisikie wanaenda kutibiwa kwa mganga wa
kienyeji, hivyo namuagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa (Dk Mtika) aagize
gari la wagonjwa lije kumchukua mtoto huyu haraka iwezekanavyo na
kumpeleka kwa matibabu ya uhakika na uangalizi na uchunguzi wa kitabibu
katika Hospitali ya Rukwa ya mkoa wa Rukwa iliyopo mjini Sumbawanga,”
alisema.
Pia alimtaka Dk Mtika kuhakikisha anamtuma mtaalamu wa magonjwa ya
ngozi kufika katika familia hiyo na kuwafanyia uchunguzi wa kitabibu,
kubaini wanafamilia wengine wapatao saba kama wanaweza kutibiwa wakiwa
nyumbani kwao; au kama watalazimika nao kutibiwa katika Hospitali ya
Rufaa ya mkoa. “Nataka maagizo yangu yatekelezwe haraka iwezekanavyo
bila kuchelewa,“ alisema.
Alieleza kuwa anasikitika pia kusikia wazazi wa mtoto huyo, kuwa
licha ya kumnyanyapaa, pia wanampiga mara kwa mara, hivyo kumwogopesha
na kusababisha awe anatoroka nyumbani mara kwa mara na kushinda na kiu
na njaa. “Inasikitisha sana kuwa licha ya mtoto huyu ambaye kweli ni
mgonjwa sana na anateseka na ugonjwa, bado wazazi wanamnyanyapaa na
kumpiga mara kwa mara,
hii haikubaliki, lazima waache tabia hii ya
kikatili mara moja,“ alieleza.
Aliwataka wakazi wa mkoa wa Rukwa, kuachana na tabia ya kuwaficha
wagonjwa nyumbani kutokana na imani za kishirikina, bali wawahishe
katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa matibabu. “Nawahimiza wakazi
wa Kata ya Kate wajiunge na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) ili
wasishindwe kutibiwa kwa kukosa fedha za matibabu, na nataka wakifika
hospitali watibiwe haraka iwezekanavyo,“ alisisitiza.
Baba wa mtoto huyo, aitwae Martin Kazumba alimweleza Zelothe kuwa
yeye ndiye alikuwa wa kwanza katika familia hiyo kuugua ugonjwa huo
miaka saba iliyopita, kisha mke na watoto wote sita, walifuata kwa
kuambukizwa ugonjwa huo. Kwa upande wake, mtoto Peter alikiri kuwa
amekuwa akipigwa mara kwa mara na wazazi wake, hivyo analazimika
kutoroka nyumbani hapo kwa kuogopa vichapo.
Kwa upande wake, Dk Mtika alieleza kuwa baada ya kumwona mtoto Peter,
upo uwezekano mkubwa kwamba ugonjwa alionao ni wa ngozi au upo
uwezekano kuwa familia hiyo imekula chakula, ambacho kimewasababishia
mzio (allergy) na siyo ugonjwa ambao unaweza kuambukiza. Akifafanua,
alieleza kuwa huo sio ugonjwa wa kuambukiza kwa sababu hakuna watu
wanaoishi karibu na familia hiyo, wameambukizwa ugonjwa huo.
“Mtoto Peter anaumwa, hali yake sio nzuri, kwanza amedhoofika kwa
njaa na kiu, mbaya zaidi anajikuna sana mwili mzima, hii inaonesha kuwa
hapati usingizi wa kutosha, amechanganyikiwa, isitoshe ugonjwa huo
umeharibu vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake. Pia hatembei vizuri,
anatembea kwa kuchechemea, jambo ambalo sio zuri, wataalamu wa ngozi
wapo, vifaa na dawa vipo, tutampeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wetu
ambapo atakuwa chini ya uangalizi wa wataalamu hao isitoshe atafanyiwa
uchunguzi wa kitabibu,“ alisisitiza.
Mratibu wa Ukoma na Kifua Kikuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Buhili aliwatoa
hofu wakazi wa kitongoji hicho kuwa ugonjwa ulioikumba familia hiyo, sio
ugonjwa wa ukoma. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nkata,
Wilbroad Feruzi alisema anawashukuru viongozi wa mkoa huo kwa kufika
katika eneo hilo na kushuhudia wenyewe jinsi mtoto Peter anavyoishi na
kutoa msaada wa kumsafirisha hadi mjini Sumbawanga kwa matibabu na
uchunguzi wa kitabibu.
Mtoto Peter aliokotwa na Paroko wa Kanisa Katoliki lililopo katika
Kata ya Kate, Padre Jofrey Kitaya, asubuhi ya Jumatatu ya Pasaka akiwa
amelala usiku kucha pembezoni mwa zahanati ya Mtakatifu Anna,
inayomilikiwa na watawa wa Kanisa Katoliki iliyopo katika kijiji cha
Kate.
Padre Kitaya alidai kuwa alipomhoji mtoto huyo, alimweleza kuwa
amelazimika kutoroka nyumbani kwao na kutembea kwa miguu umbali wa
kilomita nne baada ya kupigwa na wazazi wake na pia alidai kuwa
anawahofia wazazi wake hao. Kitongoji cha Nkata kipo umbali wa kilomita
64 kutoka mjini Sumbawanga.
0 comments:
Post a Comment