Waziri
Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe.
Hailemariam Dessalegn amemhakikishia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi yake ipo tayari
kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania
utakaosaidia kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi na kukabiliana na
umasikini wa wananchi wa nchi zote mbili.
Mhe. Hailemariam Dessalegn ametoa kauli hiyo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi wa Tanzania na Ethiopia kupitia vyombo vya habari muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili, anayoifanya kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Miongoni
mwa maeneo ambayo Mhe. Hailemariam Dessalegn alisema atatilia mkazo ni
ushirikiano katika usafiri wa anga ambapo aliahidi kuwatuma wataalamu
kutoka Shirika la Ndege la Ethiopia kuja nchini kushirikiana na
Wataalamu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuimarisha utendaji
kazi na kuikuza ATCL.
“Shirika
letu la ndege la Ethiopia ni shirika linaloendeshwa kwa faida Barani
Afrika, lina ndege 96 na linatarajia kununua ndege nyingine 42, ndege
zake zinatua katika viwanja 92 duniani kote na viwanja 42 ndani ya
Ethiopia, hivyo nitawaleta viongozi wa shirika hili ili waje
washirikiane na ATCL kuweka mkakati wa namna ya kuiendeleza ATCL na
kuiwezesha kufanya kazi kwa faida” alisema Mhe. Hailemariam Dessalegn.
Pia
alisema Shirika la Ndege la Ethiopia kwa kushirikiana na ATCL
litaufanya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es
Salaam kuwa kituo chake cha mizigo (Cargo Hub) na hivyo kuwezesha mizigo
ya ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo jirani kutumia uwanja huo
kusafirisha mizigo yake duniani kote.
Mhe.
Rais Magufuli na Mhe. Hailemariam Dessalegn ambao kabla ya kuzungumza
na wananchi walifanya mazungumzo rasmi, walisema wamekubaliana kuwa
Tanzania na Ethiopia zibadilishane uzoefu juu ya uzalishaji wa nishati
ya umeme kwa kutumia maji ambapo Mhe. Hailemariam Dessalegn aliahidi
kuwatuma wataalamu wa nchi yake kuja nchini Tanzania kutoa uzoefu wa
namna Ethiopia ilivyoweza kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kwa kutumia
maji ukiwemo mradi mkubwa unaoendelea kujengwa uitwao Grand Ethiopian
Renaissance Dam (GERD) ambao unatarajiwa kuzalisha megawatts 6,470 za
umeme.
“Mhe.
Waziri Mkuu tutafurahi sana kushirikiana nanyi katika suala la
uzalishaji wa nishati ya umeme kwa sababu hata sisi tunaweza kuzalisha
umeme mwingi katika maporomoko ya maji ya Stiegler’s Gorge yaliyopo
katika mto Rufiji” alisema Mhe. Rais Magufuli.
Viongozi
hao walikubaliana kushirikiana kufanya mapinduzi ya kilimo na mifugo,
hasa ikizingatiwa kuwa Ethiopia inaongoza kwa idadi kubwa ya ng’ombe
barani Afrika na Tanzania inashika nafasi ya pili na kwamba juhudi hizo
zitakwenda sambamba na kujenga viwanda vingi vitakavyoongeza thamani ya
mazao.
“Naamini
kuwa tukishirikiana katika kilimo na mifugo, tutaweza kutumia
teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mazao ikiwemo ngozi na nyama
na tutatumia mashirika yetu ya ndege kuyafikia masoko mbalimbali duniani
na hivyo kukuza uchumi na kuwaongezea wakulima wetu kipato” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
viongozi hawa walikubaliana kushirikiana kwa kubalishana uzoefu juu ya
namna sekta mbalimbali zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma
za benki, madini na gesi, elimu na mawasiliano hususani simu.
Mhe.
Rais Magufuli alisema ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Hailemariam Dessalegn
imekuwa ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza kuwa wakati
umefika wa kukuza biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa thamani ya
biashara kati yake ni Dola za Marekani milioni 2.24 tu.
Kabla
ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, viongozi hao
walishuhudia utiaji saini wa mikataba 3 ambayo ni Mkataba wa Mkakati wa
ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia,
Mkataba wa kuanzishwa Kamisheni ya Pamoja ya Kuduma kati ya Serikali ya
Tanzania na Serikali ya Ethiopia na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano
katika sekta ya utalii kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya
Ethiopia.
Waziri
Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe.
Hailemariam Dessalegn aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam jana asubuhi na kupokewa na mwenyeji
wake Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa na akiwa uwanjani hapo alipigiwa mizinga 19, alikagua
gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake na alishuhudia burudani ya ngoma
za asili.
0 comments:
Post a Comment