Kumekuwepo
taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa kupitia Vyombo mbalimbali vya
Habari pamoja na mitandao ya kijamii kuwa, Serikali ya Tanzania inafanya
operesheni maalum inayolenga kuwaondoa Raia wa Kenya wanaoishi nchini
bila kuwa na Vibali halali huko Wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, huku
wakimhusisha Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu katika utekelezaji wa ‘zoezi’ hilo.
Taarifa
hizi zimezua tafrani na kutishia hali ya usalama iliyopo katika mpaka
wa Tanzania na Kenya, Namanga.Tunapenda kutoa ufafanuzi kuhusu Taarifa
hizo zinazoendelea kuenezwa kuwa:-
1.Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijafanya operesheni yoyote
inayolenga kuwakamata na kuwaondoa nchini raia wa Kenya au Taifa lolote
lile wanaoishi katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kama inavyoenezewa
kwenye Vyombo vya Habari na Mitandao mbalimbali ya kijamii.
2.Shughuli
za udhibiti wa raia wa kigeni wanaokiuka Sheria za Uhamiaji nchini
hazifanywi kwa kulenga Taifa lolote lile, bali hufanywa kwa kufuata
Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi. Wahusika wanaokiuka Sheria, Kanuni
na Taratibu za uhamiaji hukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa makosa yao
binafsi na sio kwa msingi wa utaifa wao.
3.Kukamatwa
kwa raia wa kigeni ambao walibainika kuwa ni raia wa Kenya ni sehemu ya
shughuli za kawaida za Idara ya Uhamiaji kama Chombo cha Ulinzi na
Usalama katika kuhakikisha kwamba raia wa kigeni wanatambuliwa na kuishi
kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.
4.Suala
la kukamatwa kwa raia hao wa Kenya ambao walibainika kukiuka Sheria ya
Uhamiaji nchini halihusiani kwa njia yoyote ile na Serikali ya Tanzania
kulenga kuwakamata raia wa nchi yoyote na wala si agizo la Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama
ilivyoripotiwa, bali ni utaratibu wa kawaida ambao unafanywa na nchi
yoyote katika kuhakikisha kwamba ukaazi wa wageni unazingatia Sheria,
Kanuni na Taratibu za nchi husika. Kwa mfano, katika mwezi Februari
2017, Idara ya Uhamiaji imewakamata wageni 396 kutoka mataifa mbalimbali
kwa makosa ya kiuhamiaji na kuwachukulia hatua mbalimbali kwa mujibu wa
Sheria.
5.Tanzania
na Kenya tunao uhusiano mzuri sana ambao ni wa kihistoria na nchi hii
ni mwanachama mwenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa uhusiano huo,
wapo watanzania wengi wanaokwenda nchini Kenya kwa sababu mbalimbali
kama vile matembezi, biashara, masomo nk. Pia wapo raia wengi wa Kenya
wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa sababu kama hizo hizo na hatuna
tatizo nao, alimradi hawavunji Sheria za nchi yetu.
6.Mwisho,
tunatoa wito kwa Wageni wote wanaoishi hapa nchini kwa shughuli
mbalimbali kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za uhamiaji nchini. Wapo
baadhi ya wageni wanaoingia nchini kihalali, lakini wanaendelea kuishi
nchini hata baada ya muda waliopewa kuishi nchini kumalizika. Aidha,
wapo baadhi ya wageni wengine wanaoingia nchini kinyume cha sheria na
kuendelea kuishi nchini kinyume cha Sheria. Wale wanaobainika kukiuka
Sheria, Kanuni na taratibu za uhamiaji nchini watachukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria bila kujali utaifa wao.
7.Taarifa
zinazoenezwa kupitia Vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii kwamba
Tanzania inawalenga raia wa Kenya, kuwakamata na kuwaondoa nchini si
sahihi na zipuuzwe kwani zinalenga kuchafua na kuzorotesha uhusiano
mzuri uliopo baina ya nchi zetu mbili na wananchi wake, pamoja na
kudhoofisha shughuli za udhibiti wa wahamiaji haramu nchini.
8.Tunafahamu
kuwa Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa. Hivyo, tutaendeleza na
kuimarisha ushirikiano na Mataifa mengine pamoja na kuendelea kuweka
mazingira mazuri kwa wageni kuja na kuishi nchini kwa shughuli
mbalimbali, zikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, matembezi na
nyinginezo.
Imetolewa na;
KITENGO CHA UHUSIANO,
MAKAO MAKUU, IDARA YA UHAMIAJI,
BARABARA YA LOLIONDO, KURASINI,
S.L.P 512, DAR ES SALAAM.
31 MACHI, 2017.
www.immigration.go.tz
0 comments:
Post a Comment