[Sehemu
ya 3 ya Hotuba ya ndugu Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (MB) kuhusu Mapitio
na mwelekeo wa kazi za Serikali na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kwa
mwaka 2017/18]
Mheshimiwa Spika
Kuna
kijana wa kitanzania, ndugu Ben Saanane amepotea kwa zaidi ya miezi
mitano sasa. Hajulikani alipo. Wazazi wake na rafiki zake wamemtafuta na
kutoa malalamiko bila mafanikio. Wamefikisha taarifa kwa jeshi la
polisi na wamepaza sauti bila kuchoka. Kuna nyakati suala hili
lilionekana la siasa na ndio maana wengine tulikaa pembeni. Lakini sasa
ni miezi 6, kuna taarifa juu ya suala hili, nimeona nisikae kimya juu ya
hili.
Taarifa
zinatoka chini chini, sio rasmi, kwamba huyu kijana 'ametoweshwa'.
Kwamba alishikiliwa na watu wa Idara ya Usalama na amepotezwa. Jeshi la
Polisi wana taarifa za mawasiliano ya mwisho ya Ben Saanane kwa kutumia
simu yake ya mkononi, ambayo inaonekana simu ilipoteza mawasiliano akiwa
maeneo ya Buguruni siku aliyotekwa tarehe 15/16 Novemba 2016 na tangu
siku hiyo hapakuwa na mawasiliano tena.
Siku
hiyo simu yake ilisoma maeneo ya Tabata asubuhi, kisha Mikocheni na
Mwenge muda mwingi wa mchana. Saa mbili usiku alikuwa Mburahati na saa
nne usiku ilizimwa akiwa Buguruni. Polisi wanajua kuwa wenzao wa Usalama
wa Taifa ndio waliomteka kijana huyu lakini hawawezi kuchukua hatua
dhidi yao. Hivyo wameamua kukaa kimya wakiamini kuwa Watanzania
tutasahau.
Jambo
hili linasikitisha na kuumiza sana, Ben ni kijana wa kitanzania, ni
mtoto, mjomba, baba, kaka, anayo familia, siwezi hata kufikiria ni namna
gani familia yake inaumia kwa miezi hii sita bila kumuona ndugu yao,
bila kujua alipo, bila kujua hatma yake. Inaumiza sana, inaumiza mno, ni
jambo gumu sana kulivumilia, si jambo rahisi kulipuuzia na kusahau tu.
Watanzania hatupaswi kukalia kimya kuhusu jambo hili, tukisahau hili
hakuna atakayepona.
Kumekuwa
na matukio ya namna hii mabaya kabisa huko nyuma; ndugu Absalom
Kibanda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri alivamiwa na
kuumizwa vibaya sana na leo jicho lake moja halioni mwaka 2013. Pia
ndugu Yona wa Temeke alitekwa na kuumizwa na kutupwa huko mbweni jijini
Dar es salaam na hakuna mtu yeyote aliyekamatwa juu ya matukio yote
hayo. Orodha ya matukio ya namna hii ni ndefu.
Watanzania
wamesahaulishwa yote haya, Polisi mpaka Leo hawajamkamata hata mtu
mmoja juu ya yote hayo. Sababu kubwa ni ukimya wetu. Sisi wabunge
tumepewa ridhaa na wananchi wenzetu kuyasema haya, tumepewa mamlaka ya
kuihoji serikali juu ya mambo ya wananchi, na Usalama wao na mali zao ni
jambo la kwanza la msingi kabisa, wananchi wetu wakiwa na mashaka juu
ya usalama wao, shughuli za uzalishaji mali zitakuwa duni, uchumi wa
Taifa utadorora zaidi. Tunao wajibu wa kuhakikisha Usalama wa wananchi
wetu, ni wakati wa kuibana Serikali juu ya hili.
Mheshimiwa Spika,
Naomba
kulikumbusha Bunge lako Tukufu na wananchi Kwa ujumla kwamba Usalama wa
Taifa hawana mamlaka yeyote kisheria kukamata mtu yeyote yule Kwa
mujibu wa kifungu cha 5(2) cha sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1996
Kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kadhaa. Kwa hiyo Askari wa Usalama
wa Taifa waliokwenda Clouds Media na silaha, Askari wa Usalama
aliyemtolea silaha Mbunge wa Mtama, ndugu Nape, na kikosi cha utekaji na
utesaji cha Usalama wa Taifa kinachohusishwa na utekaji wa watu
wanavunja sheria ya usalama wa Taifa.
Hata
askari wa Usalama wa Taifa waliomkamata Mbunge wa Geita Vijijini, ndugu
Msukuma, Mbunge wa Nzega, ndugu Bashe na Mbunge mstaafu, ndugu Malima
walivunja sheria ya Usalama wa Taifa. Kuna viashiria vyote kuwa hali si
nzuri kabisa.
Lakini
kuna jambo moja muhimu sana juu ya jambo hili, MTAZAMO HASI wa
Watanzania juu ya Idara ya Usalama wa Taifa. Idara Nyeti, Muhimu na ya
Kuheshimiwa mno kwa Taifa letu, inaniuma leo kusimama hapa Bungeni
kuisema Idara ya Usalama wa Taifa. Mimi niko Bungeni mwaka wa 12 huu,
hatuzungumzii mambo ya Usalama wa Taifa humu bungeni, jambo hilo ni
'Taboo', lakini kwa hali ilivyo sasa imenibidi niseme.
Mambo
haya maovu yanayohusishwa na Idara hii yanaondoa uhalali wa Taasisi hii
kwa wananchi, yanaondoa heshima, hadhi na uaminifu juu ya idara hii,
yanajenga chuki na taswira hasi ya Wananchi kwa idara hii, hili si jambo
jema kwa Taifa. Ni wakati sasa wa kuchukua hatua. Ni lazima Bunge
liamke na kukomesha hali hii.
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 120(2) ya Kanuni za Bunge natoa Taarifa kwamba
nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule
kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya utekaji, uteswaji na hata mauaji
dhidi ya raia (suala la Ben Saanane likiwemo).
Pamoja
na mambo mengine, Kamati teule hiyo pia nitapendekeza iangalie namna ya
kufanya mabadiliko makubwa kwa Idara ya Usalama wa Taifa ili kuiondoa
kuwa Idara ya utesaji na badala yake kuwa idara ya kulinda Wananchi,
Rasilimali za nchi na Ulinzi wa Katiba ya nchi.
Naamini wabunge wenzangu mtaniunga mkono kwenye hili.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Dodoma
Aprili 11, 2017
0 comments:
Post a Comment